February 26, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Aliyemuua mkewe na kumchoma moto ahukumiwa kunyongwa

 

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu mfanyabiashara Hamis Said Luwongo, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mke wake wa ndoa, Naomi Marijani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Uamuzi huo umetolewa leo Februari 26, 2025 na Jaji wa Mahakama hiyo, Hamidu Mwanga, baada ya kuridhishwa na ushahidi wa mashahidi 14 na vielelezo 10 uliotolewa mahakamani hapo.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, jopo la mawakili wawili Serikali ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Yasinta Peter akisaidiana na Wakili Wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mnzava, uliomba Mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwa wanaume wote wanaowafanyia ukatili wanawake wao kwa kigezo kuwa wapo kwenye ndoa.

“Kitendo kilichofanywa na mshtakiwa ni cha ukatili na unatupa mashaka kwa wanawake waliopo katika ndoa na wanawake wanaingia katika ndoa, hivyo tunaomba Mahakama yako itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wanaume wanaotumia kigezo cha ndoa kufanya ukatili kwa wake zao” amedai wakili Mnzava.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 44/2023, Hamis, mkazi wa Gezaulole, wilayani Kigamboni, alikuwa anakabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe Naomi Orest Marijani kinyume cha kifungu cha 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, kama ilivyorejewa mwaka 2019.

About The Author

error: Content is protected !!