January 31, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Heifer yampa Sh. 25 mil kijana aliyeshinda ubunifu teknolojia ya kilimo

 

HEIFER International Tanzania leo imetangaza washindi wa Mashindano ya AYuTe Africa Challenge Tanzania 2025 awamu ya pili, ikitoa jumla ya dola za kimarekani 25,000 kwa vijana wenye kampuni changa bunifu zinazotumia teknolojia kutatua changamoto za kilimo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kupitia mashindano haya vijana 260 kutoka nchini kote walituma maombi kushiriki. Hii inadhihririsha kuwa vijana wamejikita kwenye matumizi ya teknolojia kutatua changamoto mbalimbali za wakulima wadogo wadogo ambao huchangia asilimia 80 ya uzalishaji kilimo.

Kwa kaulimbiu “Kuwawezesha Vizazi: Kutoka Urithi hadi Ubunifu,” shindano hili limeangazia suluhisho zinazoshughulikia changamoto kubwa zinazowakabili wakulima wadogo wadogo katika mnyororo mzima wa thamani wa kilimo. Mashindano haya yamethibitisha nafasi muhimu ya vijana katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini Tanzania kupitia ubunifu na teknolojia.

AYuTe Africa Challenge Tanzania, ni mradi unaotekelezwa na Heifer International na sehemu ya AYuTe NextGen Initiative, ambayo ni programu ya kuharakisha ukuaji wa biashara zinazotumia teknolojia kubadilisha uzalishaji wa chakula na kilimo barani Afrika. Mpango huu huwezesha vijana wajasiriamali wa kilimo-teknolojia kwa kuwapatia fedha ili kuongeza upanuzi wa miradi yao, pamoja na mafunzo ya uongozi, usimamizi wa miradi na usimamizi wa kifedha.

Mwaka huu, washindi waliobuni teknolojia za kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna, kudhibiti wadudu waharibifu, uzalishaji wa chakula cha mifugo kwa gharama nafuu, na matumizi ya teknolojia ya droni kwa uchambuzi wa udongo na upuliziaji wa dawa, wamegawana kiasi cha dola za kimarekani 25,000. Wajasiriamali hawa wanatarajiwa kuleta mapinduzi ya teknolojia katika sekta ya kilimo ya Tanzania.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe

Katika hotuba yake kuu, Katibu Mkuu wizara ya mifugo na uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe ambaye alikuwa Mgeni Rasmi alipongeza juhudi za Heifer International Tanzania. Alieleza kuwa mradi huu ni mkakati wa kimkakati wa kuongeza ushiriki wa vijana katika kilimo huku ukileta mageuzi kwenye sekta hiyo na kuongeza uwezo wa uzalishaji wa chakula kwa wakulima wadogo.

“Mashindano ya AYuTe Africa ni kichocheo cha kukuza biashara za kilimo-teknolojia zenye uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko, yakiwapa vijana wa Kiafrika fursa ya kutumia uvumbuzi na teknolojia kuleta mageuzi kwa wakulima wadogo kote barani,” alisema Mark Tsoxo, Mkurugenzi wa Nchi wa Heifer International Tanzania.

“Kwa kutoa fursa za ufadhili na msaada wa kimkakati, tunawasaidia vijana wajasiriamali kubadili mawazo yao bunifu kuwa suluhisho endelevu. Heifer International itaendelea kujitolea kumaliza njaa, kuunda fursa kwa vijana, na kuharakisha maendeleo ya kilimo barani Afrika kupitia suluhisho bunifu zinazoleta athari ya kudumu.”

Heifer International na washirika wake wa kimkakati wataendelea kutoa msaada wa kiufundi kwa washindi watano wa juu wa AYuTe Tanzania wa awamu ya pili, ili kuwasaidia kutekeleza na kupanua suluhisho zao za kilimo-teknolojia, hatua itakayowanufaisha wakulima wadogo wadogo na kuwasaidia kujenga ustahimilivu na kuongeza kipato chao.

Mashindano ya AYuTe Africa Challenge ni sehemu ya mpango wa bara zima unaolenga kukuza ubunifu unaoongozwa na vijana, kwa kutumia teknolojia kuwawezesha wakulima wadogo na kubadilisha kilimo barani Afrika.

About The Author

error: Content is protected !!