January 10, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

CP. Wakulyamba: Uvamizi wa maeneo hifadhi ya Taifa ya Katavi haukubaliki

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba

 

JESHI la Uhifadhi nchini limetakiwa kuhakikisha linaimarisha ulinzi katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria, ili kupambana na changamoto za uvamizi wa maeneo hayo unaofanywa na baadhi ya watu wenye nia ovu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Katavi … (endelea).

Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba alipokuwa akizungumza na Maafisa na Askari wa Jeshi hilo katika Hifadhi ya Taifa Katavi Mkoani Katavi.

CP. Wakulyamba amesema kuwa, ili kupambana na changamoto ya uvamizi katika Hifadhi hapa nchini ikiwemo Hifadhi ya Katavi yenye vivutio lukuki, mikakati madhubuti inahitajika na hivyo ameelekeza kuandaliwa kwa mikakati ya haraka iwezekavyo kudhibiti Uvamizi.

“Pamoja na kazi nzuri mnazo zifanya, nataka kuona maboresho makubwa kwenye mipango yenu iliyo madhubiti ya kupambana na wavamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kisheria. Haiwezekani maeneo yanavamiwa wakati Jeshi letu lipo na askari wapo,” alisisitiza CP. Wakulyamba.

Amesisitiza kuwa, kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Dk. Samia Suluhu Hassan katika uhifadhi inatakiwa kuungwa mkono kwa juhudi zote na hususan Maafisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi ambao wameaminiwa na Serikali kwa kupitia ajira zao

“Sisi kama Viongozi wa Wizara hatutapenda kuona wapo baadhi ya Watumishi katika Jeshi la Uhifadhi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao na kupelekea uharibifu wa urithi adhimu wa watanzania ambao umehifadhiwa kwenye Hifadhi zetu ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Katavi,” alisisitiza CP. Wakulyamba.

CP. Wakulyamba ameonya dhidi ya askari wachache wasiyo waadilifu wanaohujumu maliasili za taifa kwa vitendo vya rushwa, kwa kuruhusu mifugo kuingizwa Hifadhini au kuruhusu wachimbaji haramu wa madini kwenye maeneo yahiyohifadhiwa.

Amewaagiza viongozi wa Hifadhi zote hapa nchini, kuwachukulia hatua kali Askari wenye tatabia hizo.

Aidha CP. Wakulyamba amewasisitiza Maafisa na Askari wa Jeshi hilo kushirikiana vyema na wananchi katika uhifadhi endelevu wa Maliasili nchini kwa kuwa wananchi ni wahifadhi asilia wa maeneo waliyozaliwa.

“Maafisa na Askari wa uhifadhi ni wahifadhi kwa taaluma na Wananchi wanaoishi kuzunguka Hifadhi ni wahifadhi kwa asili,” aliongeza CP. Wakulyamba.

Akizungumzia matokeo chanya ya Uhifadhi, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Katavi, Kamishna Msaidi wa Uhifadhi, Abel Mtui, amesema ni kutokana na udhibiti mkubwa wa uwaribifu kwenye Mto Katuma uliofanywa na wahifadhi sasa umefanya mto kutiririka mwaka mzima ukilinganisha na miaka ya nyuma, jambo linalosaidia ikolojia ya Hifadhi hiyo hususani uhai wa wanyama wakiwemo Viboko.

Naibu Katibu Mkuu CP. Wakulyamba akiwa ameambata na maafisa waandamizi na wakufunzi wabobezi kutoka Jeshi la Polisi, yupo ziarani Kanda ya Magharibi kulijengea uwezo Jeshi la Uhifadhi kupitia mafunzo maalumu ya kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na utawala bora.

About The Author

error: Content is protected !!