January 7, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wazazi, walezi chanzo cha unyanyasaji kwa watoto

 

IMEELEZWA kuwa kitendo cha wazazi na walezi kutopata muda wa kukaa na watoto wao na kutumia muda mwingi kulelewa na watoto wa kazi kumechanga kwa kiasi kikubwa kutokea kwa mmomonyoko wa maadili pamoja na vitendo vya kikatili. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma ..  (endelea).

Hayo yameelezwa na mwinjilisti wa kitaifa na kimataifa Jordan Chisawino wa kanisa la Tanzania Medhodist (TMC) michese lililopo Michese Jijini Dodoma alipokuwa akihubiri katika ibada maalumu ya maombi ya malengo kwa ajili ya kuliombea taifa,uchaguzi mkuu wa 2025 na kudumu kwa amani Tanzania.

Kiongozi huyo wa Kiroho amesema kuwa wazazi na walezi wamekuwa sababu kubwa ya kuporomoka kwa maadili na kusababisha kuwepo kwa ukatili kutokana na kutokuwa na muda wa kukaa na watoto wao kuzungumza nao na kuwapa uhuru wa kusikiriza kero wanazokutana nazo.

Ameeleza kuwa jambo lingine ambalo halipaswi kujitokeza kwa mwaka 2025 ni kuwepo kwa watoto wanaoitwa wa mitaani ambao wanasababishwa na machafuko ya kifamilia na kusababisha mitafaruku inayosababisha familia kusambaratika na kufanya watoto kutawanyika mitaani.

Kutokana nanhali hiyo Mwinjilisti Jordan amesema kuwa katika mwaka 2025 kanisa la TMC limeanzisha maombi ya kufunga kwa siku 40 kwa ajili ya kuombea usalama wa Taifa, utulivu na amani katika chaguzi zote zinazotarajiwa kufanyika nchini,amani na utulivu katika ndoa na kuwaombea viongozi watoa maamuzi kutoa maamuzi sahihi yasiyo kuwa na upendeleo.

Akizungumzia masuala ya kimaendeleo amewataka watanzania kujenga tabia ya kufanya kazi kwa malengo yaliyo mema badala ya kutumia muda mwingi kukaa jiweni na kuanza kuilaumu serikali kutokana na kukosekana kwa ajira.

Mwinjilisti Jordan amesema kuwa mwaka 2025 uwe mwaka wa kutekeleza malengo ya Kiroho,Kimwili,kiuchumi na kiakili kwa nia ya kufanikisha ndoto zao za kimaisha.

“Niukweli mchungu kuwa hauwezi kutoboa kimaisha kama hautakuwa na malengo ya kufanya na hauwezi kuwa na malengo mathubuti kama malengo yako haujamshirikisha Mungu.

“Pia msitegemee kufanikiwa kwa kutegemea miujiza ya kupokea mali,majumba na magari bila kufanya kazi kwani miujiza hiyo haipo bali kinachoweza kukufanikisha ni kumwomba Mungu na kufanya kazi kwa bidii zaidi” amesisitiza Mwinjilisti Jordani.

Mwisho.

About The Author

error: Content is protected !!