December 17, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

John Tendwa afariki dunia

Marehemu John Tendwa

 

ALIYEWAHI kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa, amefariki dunia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tendwa alikutwa na mauti usiku wa kuamkia leo, wakati akipatiwa matibabu kwenye hospitali ya taifa ya Muhimbili, alikokuwa akipatiwa matibabu kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa mmoja wa wanafamilia aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina gazetini, taratibu za mazishi zinafanyika nyumbani kwa marehemu, Kibamba jijini Dar es Salaam.

Tendwa alitumikia nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa miaka 13 baada ya kuteuliwa na Rais Benjamin Mkapa. Aliondoka madarakani Agosti 2013 baada ya Rais Jakaya Kikwete kumteua Francis Mutungi, kushika wadhifa huo.

Mutungi anaendelea kushikilia wadhifa huo mpaka sasa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumuongozea muda.

Jaji John Tendwa, alikuwa mtu wa pili kushika wadhifa wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Kabla ya uteuzi wake, nafasi hiyo, ilishikiliwa na Jaji George Liundi.

Tendwa aliacha nafasi hiyo akiwa katika msuguano wa kisiasa na baadhi ya vyama, kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo aliyekuwa katibu mkuu wake, Dk. Willibroad Slaa, alitangaza kutomtambua wala kushirikiana naye.

Katika utumishi wake, Tendwa alishutumiwa mara kwa mara kwa upendeleo dhidi ya vyama vya upinzani, madai ambayo aliyakana.

Hata hivyo, madai ya ofisi ya msajili kukandamiza upinzani, yameongezeka zaidi wakati huu wa utawala wa Mutungi.

Mbali na Chadema, Mutungi amekuruzana na Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR- Mageuzi.

Baada ya kustaafu utumishi wa umma, Tendwa alikuwa akifanya kazi kama wakili wa kujitegemea akiwa na kampuni ya uwakili ya JB Advocates.

About The Author

error: Content is protected !!