December 22, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Gavu: CCM imejipanga kuwatumikia wananchi, chagueni wagombea wetu

Issa Gavu

 

KATIBU wa Halmashauri Kuu(NEC) Oganaizesheni na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Issa Gavu amesema Chama Cha Mapinduzi kimejipanga na kujidhatiti katika kuwatumikia Watanzania katika kuwaletea maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).

Gavu ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Geita wakati anazindua rasmi Kampeni za Chama hicho kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa,Vijiji na Vitongoji unaotarajia kufanyika Novemba 27 mwaka huu.

Akizungumza mbele ya wananchi hao wakiwemo wanachama wa Chama Cha Mapinduzi,Gavu amesema CCM inatambua Mamlaka ya nchi yako kwa wananchi wa Tanzania,hivyo wao kama Chama cha siasa lazima kuwaeleza mipango na dhamira yao katika kueleza waliyokusudia kuyatenda.

“Ukienda katika harakati hizi za uchaguzi huu kuna vyama 19 lakini ni Chama Cha Mapinduzi peke yetu ndio tuliojiandaa na kutengeneza kitabu maalum kinachoelezea mipango dhamira na malengo yetu katika tunayokwenda kuwafanyia Watanzania katika kukimbiza maendeleo kwa Taifa letu.

“Kwahiyo sisi wagombea wetu hawatokuja kwenu na mawazo yao kichwani watakuja kwenu na mipango,dhamira na malengo ya kutekelezwa kwa faida ya Taifa letu.Chama chetu tumejipanga kuja kwenu kuendeleza jitihada za Serikali yetu katika kuendeleza na kupeleka mbele gurudumu la maendeleo.”

Akizungumza Mkoa wa Geita amesema amezungumza na Mkuu wa Mkoa huo na kumueleza Chama Cha Mapinduzi kwa kupitia Serikali yake kimetekeleza mambo mengi yenye kuwagusa wananchi wa Geita.

“Ameniambia Geita kulikuwa na tatizo la maji sasa mkandarasi amepatikana na tunatekeleza mradi huo wenye thamani ya Sh.bilioni 124 na tayari umekamilika kwa asilimia 30 na mkandarasi anaendelea na utekelezaji wa mradi.

“Hadi kufika Juni mwakani mradi utakuwa umekamilika.Kwahiyo dhamira ya CCM na Serikali yake ni kuondoa changamoto ya maji kwa Mji wa Geita,Wilaya na Vijiji na katika hili baada ya kuona mradi utachukua muda mrefu Serikali katika kutafuta ufumbuzi imeleta gari maalum la kuchimba visima na tayari visima 48 vimechimbwa katika mkoa huo.”

Akielezea zaidi Gavu amesema ni wazi dhamira ya Serikali katika kutatua changamoto za watu wanaowangoza na wanajua maji ni muhimu katika maisha ya mwanadamu na kwa kutambua hilo Serikali imekuja na mradi huo mkubwa kumaliza changamoto hiyo na kusisitiza Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya maji na barabara.

Hivyo amesema ni vema wananchi wa Mkoa wa Geita katika uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa wakahakikisha wanachagua wagombea wa Chama hicho ambao wataungana na madiwani, Wabunge pamoja na Rais katika kuendelea kufanikisha kupatikana kwa maendeleo ya Taifa la Tanzania.

About The Author

error: Content is protected !!