November 21, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Licha ya washtakiwa kuomba Hakimu ajitoe, yeye amekataa

 

MAWAKILI wa utetezi katika kesi ya tuhuma ya kujeruhi na kutoa lugha ya matusi inayomkabili wanandoa Bharat Nathwan (57), Sangita Bharat (54) wameiomba hakimu anayesikiliza kesi hiyo ajitoe kwa sababu hawana imani nae kutokana na maamuzi anayoyato. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Aidha, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Aaron Lyamuya amekataa kujitoa kusikiliza kesi hiyo kwa madai kuwa mmoja wa mawakili wa washtakiwa hao, Gabriel Mnyele hakutoa sababu ya msingi ya yeye kujitoa.

Hata hivyo, Wakili mwingine wa washtakiwa hao Edward Chuwa amedai kuwa atakwenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi huo wa hakimu kukataa kujitoa kwa sababu bado hawana imani nae kwa kutupilia mbali pingamizi zao mbili.

Mahakama ilifikia kutoa uamuzi huo, baada ya Wakili Mnyele kupinga shahidi watano wa upande wa mashtaka Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (Assistant Inspector) Calvin (36) kutoa ushahidi wake kwa kile alichokiona eneo la tukio kwenye picha za CCTV ( CCTV Footage).

Hata hivyo, shahidi hakuweza kumaliza kutoa ushahidi wake, kutokana na ubishani uliyotokea kwa Wakili Mnyele kudai kuwa hawezi kuelezea kile alichokiona kwenye CCTV ni suala la ushahidi wa kieletroniki, kwa hiyo anatakiwa awasilishe kwanza picha hizo.

Hali ambayo ilisababisha Hakimu Lyamuya kutoa uamuzi kuhusiana na suala hilo, ambapo alisema alichokuwa anakizungumza shahidi hakuna ushahidi wa kieletroniki, hakuna kinachomnyima shahidi kuelezea alichokiona kama mpelelezi.

“Kama hiyo CCTV Footage itakapoletwa Mahakama ndiyo itapata nafasi ya kulinganisha maneno ya shahidi na kinachoonekana katika kamera,”alisema Hakimu Lyamuya

Uamuzi huo, ulisababisha upande wa utetezi kukataa kuendelea na shahidi huyo kwa madai kwamba hawana imani na hakimu huyo, kwa sababu kila walipotaka shahidi kuleta CCTV Footage mahakama anatupilia mbali pingamizi lao.

Awali, walitaka mlalamikaji Kiran Lalit kuwasilisha ushahidi huo wa kuonesha jinsi alivyosukumwa ndani ya ndoo iliyokuwa na mchanganyiko wa saruji, lakini mahakama iliingilia kati na kudai kuwa wafuate taratibu kama wanataka kielelezo hicho.

Kesi imeahirishwa hadi Desemba 3,2024 saa tano asubuhi, Shahidi namba tano Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (Assistant Inspector) Calvin (36) ataendela kutoa ushsiwake.

Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania asili ya kihindi wanaoishi Mtaa wa Mrima – Kisutu, jengo la Lohana Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashtaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa Nathwan anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jingo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo la saruji iliyochanganywa.

About The Author