WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ameahidi kuendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto katika Chuo cha Maji ambapo amewataka watendaji wa sekta ya maji walioko mkoani Dar es Salaam kuhudhuria kikao kazi katika chuo hicho siku ya Alhamisi tarehe 14 Novemba 2024, kwa ajili ya kujadili changamoto hizo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Waziri Aweso ameyasema hayo katika Mahafali ya 48 ya Chuo cha Maji ambayo yamefanyika leo Jumatano tarehe 13 Novemba 2024, ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam ambapo alikuwa Mgeni Rasmi.
“Naibu Katibu Mkuu upo, mtu wa Mfuko wa Maji upo, twendeni tukakae tukakitembelee chuo chetu cha maji, tuone mafanikio yao, tuone na changamoto yao. Sehemu ambapo kunahitajika kuchukuliwa hatua tunachukua hatua, sehemu ambapo panahitaji nguvu zaidi mimi nitapokea na kisha kuwasiliana na Rais kuhakikisha anatusaidia na kukisaidia Chuo cha Maji”, amesisitiza Aweso.
Aidha amesema kwamba serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya elimu na hasa kwenye Chuo cha Maji kwa kukiboresha kwa nyanja mbalimbali ukilinganisha na miaka iliyopita.
“Changamoto iliyokuwa mbele yetu ya kufanya mageuzi katika chuo cha maji ilikuwa ni suala la ufinyu wa bajeti..Kiongozi ni maamuzi, tukasema hapana, suala la bajeti haliwezi likatuzuia sisi kufanya mageuzi ndani ya Chuo cha Maji,” amesema Aweso.
Katika hatua nyingine ameridhishwa na namna Chuo cha Maji kinavyojipanga kutekeleza majukumu yake katika sekta ya maji, akiipongeza bodi ya chuo hicho kwa kutekeleza majukumu ya kuwa washauri katika chuo hicho na akiamini kuwa majukumu hayo yataendelea kutekelezwa kwa masilahi ya chuo na taifa kwa ujumla.
Halikadhalika ametoa wito kwa wazazi na walezi nchini kuwekeza katika elimu ya watoto wao.
“Mimi ni muumini mkubwa wa elimu, ninaamini kabisa kupitia elimu mtoto wa mamantilie anaweza kuwa mhandisi tegemezi katika taifa hili, katika nafsi yangu ninaamini mtoto wa masikini kabisa katika taifa hili anaweza kuwa Mkuu wa Chuo cha Maji kupitia elimu”, amesema Waziri Aweso.
ZINAZOFANANA
Waziri Jafo akagua maandalizi miaka 60 ya CBE
TRA, Wafanyabiashara Kariakoo kufanya Bonanza la pamoja J’pili
TMA yatoa taarifa ya uwepo wa Kimbunga Dikeledi, pwani ya Msumbiji