November 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Ujenzi wa barabara, madaraja Babati kufungua Utalii

 

IMEELEZWA kwamba ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja unaofanywa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani Babati unaenda kufungua shughuli za utalii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Babati, Manyara … (endelea).

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Emmanuella Kaganda ameeleza hayo alipofanya mahojiano na waandishi wa habari ofisini kwake wilayani humo, Mkoani Manyara hivi karibuni.

Kaganda amesema kufunguka kwa mtandao wa barabara kumeweza kuvutia watalii katika mbuga za Taifa za Tarangire na Manyara, utalii wa kitamaduni, Ziwa Manyara pamoja na milima ambayo wananchi hufanya shughuli za kitalii.

“Babati inaenda kufunguka kwani mtandao wa barabara unaendelea kuongezeka kwa kuwa na Kilomita 1,548.792 ambapo Mji wa Babati una Km. 595.102 na Halmashauri ya Babati Km. 953.69,” alisema na kuendelea,

“Hakika kazi kubwa inafanyika na Serikali ya Awamu ya Sita kwani Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kutupatia pesa za kuwekeza kwenye miundombinu,” alisisitiza.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 TARURA wilaya ya Babati imepanga kutumia zaidi ya shilingi bilioni 4.9 kwaajili ya kuchonga barabara, kutengeneza barabara za changarawe, kujenga madaraja na Papu Kalavati.

Aidha, amesema katika kipindi cha miaka mitatu wamepokea jumla ya Sh. 12 bilioni kwaajili ya kuimarisha mtandao wa barabara ambapo awali TARURA walikuwa wakipokea bilioni 1 hivyo ongezeko la bilioni 3.5 ni ongezeko kubwa katika wilaya hiyo.

“Ongezeko hili sio kidogo na tumeona namna Rais alivyoamua kuibadilisha Babati yetu,” aliongeza kusema.

Hata hivyo Kaganda alisema katika matengenezo hayo wanatarajia kufunga taa zipatazo 90 katika barabara ya kuelekea hospitali ya wilaya ya Mrara ili kulinda usalama wa wananchi wakati wakielekea kupata huduma nyakati za usiku.

Hivyo ametoa rai kwa wananchi wa wilaya hiyo kuitunza miundombinu inayojengwa na Serikali na kuepuka kufanya shughuli za kilimo kandokando ya barabara na kupitisha majembe yanayokokotwa na wanyama ili kuepuka mmomonyoko wa ardhi.

Pia aliwataka wananchi kusafisha mitaro iliyopo mbele za nyumba zao, kutokutupa taka hovyo na hivyo kutunza mitaro ya maji hususani kipindi hiki cha mvua ili kuepuka mafuriko na magonjwa mbalimbali yanayotokana na uchafu.

Naye, Hamis Rajabu Mkazi wa Mtaa wa Mrara amesema madaraja waliyojengewa katika barabara hiyo ambayo ni kiunganishi kati ya Babati Mjini na Vijijini yameweza kuwaondolea kero mbalimbali zilizokuwa zikiwakabili hususan kipindi cha masika ambapo magari na vyombo vingine vya moto vilikuwa vikipita kwa kupokezekana.

About The Author