MAKAMU wa Rais, Dk. Philip Mpango amelipongeza Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) kwa kuratibu vyema tuzo za wenye viwanda tangu kuanzishwa kwake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Alitoa pongezi hizo leo jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa tuzo za Rais kwa Mzalishaji Bora wa Mwaka Viwandani zinazoratibiwa na CTI), President Manufacturer of the Year Award (PMAYA).
Katika tuzo hizo Kampuni ya Sigara TCC iliibuka mshindi wa kwanza ikifuatiwa na kampuni ya bidhaa za plastiki ya Plasco Limited na kampuni ya mabati ya ALAF Limited.
Makamu wa Rais alisema tuzo hizo zimekuwa chachu kubwa ya maendeleo ya viwanda ambavyo vimekuwa nguzo kubwa ya ukuaji wa uchumi kutokana na kuzalisha ajira nyingi.
Alisema sekta ya viwanda ni chimbuko la maendeleo ya nchi na ina fursa kubwa ya kukua haraka na kutengeneza fursa za ajira na kuchochea bunifu na maendeleo ya teknolojia.
Alisema sekta ya viwanda ni eneo muhimu la kuongeza ajira nchini na kuliongezea taifa fedha za kigeni na inamchango kwenye ukuaji wa sekta zingine kutokana na kuzalisha bidhaa zinazouzwa nje na ndani ya nchi.
“Licha ya umuhimu mkubwa wa sekya ya viwanda kwenye ukuaji wa pato la taifa, mchango wa sekta hiyo hapa nchini bado ni mdogo sana kwa hiyo wenye viwanda wanapaswa kupambana kukuza sekta hiyo,” alisema.
“Nakumbuka mwaka 20021 niliwapa changamoto na leo hii narudia tena kuwataka muongeze mchango wenu katika mapato ya fedha za kigeni kwenye uchumi wetu na kwenye ajira rasmi,” alisema
Alisema moja ya changamoto ya ukuaji wa viwanda ni pamoja na kushindwa kupata mikopo ya gharama nafuu, uhaba wa rasilimali watu wenye ujuzi, matumizi ya teknolojia yaliyopitwa na wakati, miundombhinu hafifu na vikwazo visivyo vya kodi.
“Sasa katika kukabiliana na changamoto hizi kunahitajika jitihada za pamoja za wadau na kuongeza tija na kuongeza ushindani kwenye sekta ya viwanda mzalishe bidhaa ambazo ni nyingi na ambazo zitashindana kwenye masoko ya nje,” alisema Dk Mpango.
“Serikali inaendelea kufanya jitihada kubwa kuimarisha sekta ya uchukuzi ikiwa ni pamoja na kuimarisha usafiri wa anga, usafiri wa treni na ndiyo mara leo nimelala Dodoma na muda huu niko hapa Dar es Salaam,” alisema.
Alisema katika jitihada za kukuza maendeleo ya viwanda serikali inaendelea kusimamia ukamilishaji wa ujenzi wa bwawa la umeme la Julius Nyerere (JNHPP), ambapo mpaka sasa ujenzi wake umeshafikia asilimia 99 na mitambo imeshawashwa na kuzalisha umeme.
Makamu wa Rais aliwapongeza wafadhili wa tuzo hizo ambao ni Bonite Bottlers Ltd, Alaf Ltd, GF Trucks, TCC, Kilimanjaro Cables, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari (TPA), Motisun Group na Alliance Life Insurance.
Aliwataja wafadhili wengine ambao ni Mati Super Brand Ltd, SBL, Bakhresa Group na Watercom.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alipongeza Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI) kwa namna ambavyo imekuwa ikisimamia utoaji wa tuzo hizo tangu kaunzishwa kwake.
Rais wa CTI, Paul Makanza aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa namna ambavyo imekuwa ikiendelea kuwawekea mazingira mazuri wawekezaji na kusikiliza kero zao.
“Tunaomba utufikishie salamu zetu kwa mhesnimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, wawekezaji na wenye viwanda lazima tumshukuru kwa kuwa msikivu, tulikuwa na changamoto nyingi sana lakini tumekaa na serikali na nyingi zimepatiwa ufumbuzi,” alisema Makanza.
ZINAZOFANANA
Chuo Kikuu cha Marekani kutunuku shahada ya Udaktari kwa watanzania wanne
Serikali yatia nguvu ubunifu na utafiti kuzikabili changamoto za uchumi na jamii
Nondo atelekezwa Magomeni akiwa mahututi