December 25, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

‘Dk Manguruwe’ aburuzwa kortini kwa uhujumu uchumi

 

MFUGAJI maarufu nchini pia Mmiliki wa Kampuni ya Vanilla Internation Ltd Simon Mkondya (40), ‘Dk Manguruwe’ na mwenzake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 28. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Katika kesi hiyo, Mkondya na Mwenzake Rweyemamu John ambaye ni Mkaguzi kampuni hiyo wanakabiliwa na mashtaka 19 ya ulaghai kwa kutumia upatu na mashtaka tisa ya kutakatisha fedha kwa kununua viwanja vilivyopo huko Njombe eneo la Idunda.

Leo tarehe 5 Novemba 2024 mbele ya Hakimu Mkazi Aaron Lyamuya, Wakili wa serikali Job Mrema amesema hati ya mashtaka na kudai kuwa washtakiwa walitenda kosa hilo kati ya January Mosi 2020 na Desemba 2023 jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa katika kipindi hicho Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla pamoja na mkaguzi wake huyo walifanya biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu kuwa ukitoa kiasi chochote cha pesa utapata faida mara tatu ya kiasi ulichotoa.

Inadaiwa washitakiwa walijipatia jumla ya Sh Milioni 92.2 kutoka kwa watu kumi na tisa tofauti ikiwa kila mmoja alimpatia kiasi chake cha fedha akimuahidi kuwa fedha hizo zingezaa mara tatu ya zile alizotoa.

Katika mashtaka tisa ya utakatishaji mshtakiwa Mkondya peke yake anadaiwa katika kipindi hicho hicho, akiwa ndani ya Mkoa wa Dar es salaam alijipatia jumla ya viwanja tisa vitalu namba Ab vilivyopo eneo la Idunda Mkoani Njombe huku akijua kuwa viwanja hivyo ni mazalia ya kosa tangulizi la upatu.

Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi ambazo kwa kawaida husikilizwa mahakama Kuu ama kwa kupewa kibali kutoka kwa mkurugenzi wa mashtaka DPP.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 19,2024 itakapokuja kwa ajili ya kutajwa. Mshtakiwa amerudishwa rumande.

About The Author

error: Content is protected !!