November 21, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali yapongeza mafanikio ya kitaaluma shule ya Hazina

 

SERIKALI imeipongeza Shule ya Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam kutokana na mafanikio ya kitaaluma na mchango wake kwa serikali katika sekya ya elimu.

Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Mdhibiti Ubora wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Albert Mutalemwa wakati wa mahafali ya shule ya awali na msingi Hazina jijini Dar es Salaam.

Kwenye matokeo ya shule hiyo yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA), wanafunzi wote 27 wa shule hiyo walipata alama A kwenye masomo yote.

Alisema kiwango kikubwa cha maarifa walichoonyesha wanafunzi wa shule hiyo kwenye maonyesho mbalimbali ya kitaaluma kinadhihirisha elimu bora inayotolewa na shule hiyo.

Alisema wanafunzi hao wameonyesha umahiri wa hai ya juu kuelezea masuala mbalimbali yakiwemo ya sayansi na tiba ya magonjwa mbalimbali kana kwamba ni madaktari.

“Walimu kwa upande wao wanafundisha vizuri sana na mmeona namna gani watoto wameelezea kwa umahiri wa hali ya juu hapa lakini wazazi mnapokuwa nyumbani hakikisheni watoto wanakuwa na maadili mema na waepuka kukaa na makundi yanayoweza kuwasababishia kupata tabia za ovyo,” alisema

“Nimeambiwa hapa kwamba kuna wageni kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) sasa kuwepo kwa wageni hawa kunaonyesha kwamba shule hii iko vizuri sana kwenye uhusiano wa kimataifa ambayo inaweza kuwasaidia wanafunzi wa shule hii kupata fursa za kimataifa,” alisema

Wanafunzi wa shule hiyo walionyesha umahiri wa hali ya juu kwenye maonyesho mbalimbali ya kitaaluma kiasi cha kuwashangaza wazazi na wageni waalikwa waliohudhuria hafla hiyo.

Miongozi mwa maonyesho waliyofanya ni kuonyesha namna ya kutibu ugonjwa wa ini na kutoa maelezo ya kina ya namna mtu anavyoweza kulinda afya yake kwa kubadili mtindo wa maisha na kula kwa kuzingatia afya.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Omari aliwashukuru wazazi kwa kuwaamini na kuwapa watoto wao wawafundishe na aliahidi kuwa wataendelea kuhakikisha shule hiyo inafanya vizuri kwenye mtihani ya kitaifa.

“Tumekuwa tukifanya vizuri sana na kushika nafasi ya kwanza kwenye mitihani kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na kitaifa kama mlivyoona matokeo ya mwaka huu lakini nawahakikishia wazazi hatutabweteka na badala yake tutahakikisha tunabaki kwenye ubora ule ule,” alisema

Alisema wanafunzi wa shule hiyo hivi karibuni walialikwa kutoa mada kuhusu mashirika yaliyo chini ya Umoja wa Mataifa (UN), ambapo Waziri wa Ulinzi aliyekuwa mgeni rasmi aliwapongeza kwa kujiamiini na kutoa mada ambayo iliwasisimua wageni waalikwa.

“Wanafunzi wa Hazina wamefundishwa kujiamini na kuzungumza kwa lugha ya Kingereza kwa ufasaha mbele za watu na ndiyo sababu walichaguliwa kwenda kwenye siku ya Umoja wa Mataifa, walizungumza na walikonga nyoyo za wageni waalikwa,” alisema.

About The Author