December 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wafugaji watamba kuwaweka viongozi wa wilaya mfukoni

 

WAFUGAJI wa kata ya Gwata wilayani hapa, wametamba kuwa hakuna anayeweza kuwafanya chochote juu ya madai ya wakulima wa eneo hilo, wanaolalamikia mazao yao kuliwa na ng’ombe wa wafugaji hao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kibaha, Pwani … (endelea).

Kibaya zaidi, wakulima hao wanalalamikia fidia wanayolipwa kwa uharibifu wa mazao yao kuwa ni ndogo na wakati mwingine wafugaji wanaotakiwa kulipa, wanagoma na hakuna anayeweza kuwachukulia hatua.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwandishi wa Habari hizi alifika Gwata na kukutana na baadhi ya wakulima walioharibiwa mazao ambapo kilio chao kilikuwa dhidi ya wafugaji na namna wanavyotamba bila kuchukuliwa hatua kwa uharibifu unaofanywa na mifugo yao.

Wakulima hao wanalalamika kuwa wafugaji wamekuwa na jeuri, kiasi kwamba wanatamba bila woga kuwa hakuna mtu anayeweza kuwafanya chochote.

Baadhi ya wakulima waliofanyiwa tathimini na uharibifu wa mazao yao na kiasi cha fidia wanachopaswa kulipa ni pamoja na Andrea Lubote (115,000/-), Mohammed Waziri (133,000/-), George John (172,000/-), Tausi Mgonge (115,000/-), Bernad Zugazuga, (134,000/-), Maua Kibwana (127,000/-), Asha Mponda (680,000/-), Haji Machupa (152,000/-), Iddy Kisatu (107,000/-), George Gervas (155,000/-), Peter John (175,000/-), Simon Mangole (153,000/-), Leonard Daud (125,000/-) na wengine wengi.

Akizungumza kwa uchungu dhidi ya madhila hayo, Lubote alisema mifugo wameingia shambani kwake na kuharibu mazao yake na kusababisha hasara kubwa.

“Amekuja mthamini, amefanya tathimini, akaniletea gharama ya fidia ninayopaswa kulipwa, nimekuta ameandika Sh 155,000. Yaani shamba zima la mihogo zaidi ya ekari mbili, limeharibiwa na ng’ombe, fidia yake Sh 155,000, hiki ni kiasi kidogo sana, hakilingani na thamani ya mazao yangu yaliyoharibiwa,” alisema Ubote.

Aliongeza kuwa kibaya zaidi, katika fedha za fidia zinazolipwa, Sh 20,000 zinalipwa kwa waliozingira mifugo na kuiswaga hadi kwa mmiliki, ili ajulikane na aambiwe fidia anayopaswa kulipa.

Aboubakari Kunenga, Mkuu wa Mkoa wa Pwani

Alisema Sh 20,000 zinatolewa kwa Kamati ya Utatuzi wa Migogoro ya Kata ambao huwa wanakuja kuangalia eneo lililoharibiwa na Sh 10,000 zinatolewa kwa mtathimini.

“Fikiria umeandikiwa fidia ya Sh 155,000 ambayo ikienda kwa mfugaji bado anaweza kuikataa na akalipa kidogo, lakini hata hicho kidogo akilipa, Sh 50,000 zinakwenda kwa hawa niliwaotaja.

“Wafugaji wanatunyanyasa sana, wakiamua hata hiyo fidia ndogo hawalipi, wakiitwa Polisi hawaendi au anaweza kujibu nitakuja kesho au siku nikiwa na nafasi na Polisi haiwezi kufanya chochote, ukitaka kwenda mahakamani, gharama ya kugongewa mhuri tu ni Sh 30,000, kwenda kufungua kesi nako ni gharama nyingine, lakini ile nenda mahakamani, kesi inaweza kuchukua zaidi ya mwaka, huwezi kuendelea unaacha kwa sababu huwezi kumudu gharama,” anasema Lubote.

Mkulima huyo alionya kuwa endapo Serikali itaendelea kuwaacha wafugaji watambe na mifugo yao kuendelea kuharibu mazao bila kuchukuliwa hatua, kuna hatari ya kutokea vurugu.

“Mimi siku walipoingia shambani kwangu, nilitoka na panga niwakatekate ng’ombe hao, lakini mwanangu alinisihi sana kupunguza hasira, vinginevyo leo tungeongea lugha nyingine, tumechoka kunyanyaswa na wafugaji kwa sababu ya fedha zao.

Zugazuga alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge kufika eneo hilo kushuhudia kilio cha wakulima badala ya kusikiliza viongozi wa kata, kijiji na hata wilaya ambao alidai wamewekwa mifukoni mwa wakulima.

Akitoa ufafanuzi wa madai ya wakulima, Ofisa Kilimo Kata ya Gwata, Pili Thabit, alisema fidia wanazotoa kipindi hiki cha ukame ni sahihi, kwani mazao yameharibiwa na ukame.

“Ukifika huku ‘site’ utaona. Huwezi kutoa fidia kubwa kwa mazao ambayo tayari yameshakumbwa na ukame. Ingekuwa wakati wa masika, mfugo mmoja tu ukiingia shambani ni Sh 50,000. Hapo hujaangalia ameharibu nini. Lakini kipindi hiki tunachofanya ni sahihi na hakuna mfugaji aliye juu ya sheria.

Pili, wakulima wasioridhika na fidia wanayotoa Serikali, anapaswa kupeleka malalamiko yake mahakamani ambako sisi tumekuwa tukiitwa kutoa ushahidi.

“Hakuna mfugaji aliye juu ya sheria na kila tunachofanya kipo kwa mujibu wa sheria. Madai kwamba kiasi kingine cha fidia wanalipwa watu wengine, hilo mimi sijui maana kazi yangu ni kufanya tathimini na kuelekeza kiasi cha fidia inayopaswa kulipwa,” alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kunenge alipoulizwa kwa njia ya simu juu ya tatizo hilo, alisema hata taarifa na kwamba atafuatilia kujua nini kinaendelea.

 

About The Author

error: Content is protected !!