BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) ambae ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya NBC jana iliipamba mechi ya Simba na Yanga maarufu kama ‘Kariakoo Derby’ kwa kuandaa matukio kadhaa kwa ajili ya wapenzi wa mchezo huo pamoja na wateja wa benki hiyo. Matukio hayo yalilenga kutoa fursa kwa wadau hao kukutana pamoja ili kuutazama na kufurahia vizuri zaidi mchezo huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Pamoja na kuandaa chakula cha mchana kwenye hoteli ya Four Points iliyopo jijini Dar es Salaam mahususi kwa baadhi ya wateja wake wanaoshabikia timu hizo mbili, mdhamini huyo pia aliwawezesha wateja hao kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa wakiwa kwenye msafara maalum ili kushuhudia mechi hiyo wakiwa kwenye jukwaa la VIP. Mechi hiyo iliisha kwa ushindi wa goli 1-0 iliyoupata timu ya Yanga SC dhidi ya Simba SC.
Shughuli zote hizo ziliongozwa na maofisa waandamizi wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Fedha, Rayson Foya ambae pia alipata wasaa wa kukabidhi tuzo kwa Mchezaji Bora (Man of the Match) wa mchezo huo, Maxi Nzengeli kutoka klabu ya Yanga, tukio lililoshuhudiwa na maelfu ya mashabiki waliofika uwanjani hapo na wengine wengi waliokuwa wakitazama mchezo huo kupitia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni.
Zaidi, benki hiyo iliandaa ‘screen’ kubwa kwenye baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo kwenye Mgahawa maarufu wa Hoppipola uliopo Masaki ili kutoa fursa kwa mashabiki wengi zaidi ambao hawakupata wasaa wa kufika uwanjani waweze kushuhudia vizuri mechi hiyo kubwa zaidi nchini Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
Awali akizungumzia hatua hiyo wakati wa hafla ya chakula cha mchana na wateja hao, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa benki ya NBC, Godwin Semunyu alisema ni muendelezo wa maadhimisho ya mwezi wa huduma kwa wateja wa benki hiyo sambamba na jitihada za benki hiyo kama mdhamini mkuu wa ligi hiyo kuutumia mchezo pendwa wa soka kujenga mashusiano yake na wateja wake sambamba na kuchochea mapenzi ya wadau hao kwa vilabu vyao na mchezo huo kwa ujumla.
“Udhamini wetu kwenye mchezo huu pendwa zaidi nchini na duniani kwa ujumla umekuwa hauishii tu kulenga katika kuboresha ligi hizi tatu tunazozidhamini bali pia tumekuwa tukihakikisha wadau wetu wote muhimu wakiwemo wafanyakazi, uongozi wa benki na wateja wetu wanakuwa sehemu ya mchezo huu kwa kushiriki moja kwa moja kwenye matukio mbalimbali ikiwemo kushuhudia mechi kubwa kama hizi,’’ alisema Semunyu.
Alisema benki hiyo inaendelea kubuni mikakati mikubwa zaidi ya kuiboresha ligi hiyo ili kufikia malengo ya udhamini wake ambayo ni pamoja na kukuza vipaji na viwango vya soka nchini, kuchochea ajira kupitia michezo, kuongeza ushindani baina vilabu shiriki na kuongeza hamasa ya mchezo huo nchini.
“Kila mtu ni shuhuda wa mapinduzi makubwa ambayo tayari benki ya NBC tumeyafanya katika misimu hii mitatu iliyopita ya udhamini wetu kwenye ligi Kuu ya NBC na mwaka mmoja wa udhamini wetu kwenye ligi ya Championship na ligi ya Vijana,’’ alisema.
Mbali na kuchochea ushindani kwenye ligi hizo kupitia udhamini ulioviwezesha vilabu shiriki kufanya usajili mzuri, imeshuhudiwa mdhamini huyo pia akitoa huduma muhimu za kibenki kwa timu hizo ikiwemo bima ya afya, mikopo ya usafiri kwa timu na kushiriki katika kudhamini hafla mbalimbali za mchezo huo zikiwemo zile za kukabidhi vikombe vya ubingwa pamoja na kudhamini tuzo mbalimbali za mchezo huo.
ZINAZOFANANA
Shindano la Mabingwa Expanse kukupa mamilioni Sikukuu hii
Cat Purry Kasino mtandaoni makulipo makubwa
Michuano ya Expanse kukupa mkwanja msimu huu wa Sikukuu