November 21, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mtaalamu bingwa wa nyonga na magoti wa Uingereza atua Dar

 

MTAALAMU bingwa wa upasuaji wa nyonga na magoti kutoka hospitali ya Qeen Elizabeth ya Uingereza Profesa Mamoun AbdelGadir, amewasili jijini Dar es Salaam kwaajili ya kambi ya matibabu ya siku tano kwa watanzania. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Daktari huyo kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani atafanya upasuaji huo kwenye kambi itakayofanyika katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila kuanzia leo Jumatatu.

Aliwasili leo katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo alipokelewa na wafanyakazi wa Global Medicare ambao wameratibu kambi hiyo kwa kushirikiana na Muhimbili Mloganzila.

Akizungumza kwenye mapokezi hayo, Meneja Mkuu wa Global Medicare, Daniel Lazaro, alisema wamefurahi kuona amefika salama nchini Tanzania na kwamba ujio wake utakuwa wa manufaa makubwa kwa watanzania wenye matatizo ya nyonga na magoti.

“Tumefurahi kuona umefika salama na tunatarajia watanzania wengi watanufaika na ujio wako kwenye kambi hii ya siku tano itakayoanza katika hospitali ya Muhimbili Mloganzila kuanzia Jumatatu,” alisema

Naye Profesa Gadir aliishukuru serikali ya Tanzania na taasisi ya Global Medicare kwa kuratibu vyema safari yake ya kuja nchini Tanzania na aliahidi kutoa huduma bora kwa wagonjwa watakaojitokeza kwenye kambi hiyo.

“Natarajia tunashirikiana vizuri sana na wataalamu wenzangu wa hapa nchini kwenye kambi hii ya siku tano na kwa huduma hii natarajia tutaongeza chachu ya ushirikiano wa nchi zetu na tutabadilishana uzoefu wa kufanya upasuaji wa aina hii kwa wataalamu wetu,” alisema.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali ya Mloganzila, Goodlove Mfuko, alisema hivi karibuni kuwa maandalizi yote yamekamilika na kwamba kwenye kambi hiyo watashirikiana na mtaalamu huyo.

“Mtaalamu huyu atashirikiana na madaktari bingwa ambao ni wataalamu wa mifupa na ajali hapa Mloganzila, hii itakuwa mara ya pili kutoa huduma kama hii kwani mara ya kwanza tuliwafanyia upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti wagonjwa 170 kwa mafanikio makubwa,” alisema

“Kwa hiyo kwenye kambi hii ambayo ni ya pili tutashirikiana na daktari huyu mbobezi kutoka Uingereza kupata uzoefu ili tuweze kuboresha zaidi huduma zetu hapa Muhimbili Mloganzila,” alisema

Aliwashauri watu wenye matatizo ya nyonga na magoti wafike Mloganzila kwaajili ya kupewa hiyo huduma ya kubadilisha nyonga na magoti kutoka kwa mtaalamu huyo wa Uingereza .

Aron Mwamyanda ambaye alifanyiwa upasuaji wa goti kwenye kambi iliyopita Mloganzila alisema aliugua magoti kwa miaka mitatu na alizunguka hospitali nyingi bila mafanikio.

“Nilienda hadi kwa waganga wa jadi lakini sikufanikiwa lakini mtoto wangu mmoja aliposikia kuna wataalamu wa magoti na nyonga hapa Mloganzila alinileta. Nilikuja wakanipiga wakasema hali yangu ni mbaya wakanipa gharama wakanitibia,” alisema

“Baada ya kunifanyia upasuaji hali yangu imekuwa tofauti kabisa kwasababu naweza kufanya mambo mengi ambayo awali sikuwa na uwezo wa kuyafanya na natarajia nitarejea kwenye hali yangu ya kawaida,” alisema

About The Author