Bunge la Seneti nchini Kenya, limeanza kujadili hoja ya kumwondoa madarakani, Naibu Rais wa nchi hiyo, Rigathi Gachagua, leo Jumatano tarehe 16 Oktoba 2024.
Mjadala huo wa siku mbili kuanzia leo, unakuja wiki moja baada ya wabunge kupiga kura ya kumwondoa kwenye wadhifa huo Jumanne ya wiki iliyopita, akituhumiwa kwa makosa 11.
Bunge hilo litachunguza mashtaka dhidi ya Gachagua na kusikiliza ushahidi kutoka pande zote.
Gachagua alitimuliwa na bunge Jumanne tarehe 08 Oktoba 2024, baada ya wabunge 281, kupiga kura ya kuunga mkono kuondolewa kwake ofisini.
Kiwango kilichowekwa na katiba ni angalau wabunge 233.
Katika kura za wiki iliyopita, wabunge 281 waliunga mkono hoja hiyo, na 44 waliipinga; na kufikia theluthi mbili ya kura zilizohitajika ili kupitisha uamuzi wa kumuondoa ofisini.
Baada ya kusikiliza pande zote, Seneti litatoa uamuzi wa mwisho ndani ya siku 10. Ili atimuliwe, theluthi mbili ya kura za wabunge wa seneti inahitajika.
Baadhi ya tuhuma zinazomkabili Gachagua ni tuhuma za ufisadi, kumhujumu rais na kuendeleza mgawanyiko wa kikabila, madai ambayo ameyakana akisema anafanya kazi kwa maslahi ya Wakenya.
Mjadala wa Seneti unakuja siku moja baada ya Mahakama Kuu ya Kenya, kutupilia mbali ombi la mwanasiasa huyo, aliyetaka mhimili huo uzuie kujadiliwa kwake na Bunge la Seneti, akidai kuwa hoja ya kumtimua ilitokana na madai ya uongo yaliyochochewa kisiasa.
Mahakama imetupa hoja ya Gachagua, ikieleza kuwa ni mchakato wa kikatiba ambao hauwezi kuingiliwa na mhimili mwingine.
ZINAZOFANANA
Wagombea wasioridhishwa na uteuzi waweke pingamizi
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA Dar
Wahariri wamparura Waziri Silaa kwa kuwakacha