December 24, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Chalamila aipongeza Puma kupunguza matumizi ya nishati chafu Dar

 

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema uamuzi wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania kutoa mitungi 1,000 ya gesi katika mkoa huo kwa ajili ya kuwapatia Mama Lishe na Baba Lishe kunakwenda kuchochea kasi ya safari ya kuzuia matumizi ya nishati chafu ya kuni na mkaa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza leo Oktoba 11, 2024 katika viwanja Vya Biafra, Kinondoni Mkoani Dar es Salaam alipokuwa akipokea mitungi hiyo iliyotolewa na Kampuni ya Puma Energy Tanzania, Chalamila amesema uamuzi huo umekuja wakati sahihi kwani dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imedhamiria wananchi kutumia nishati safi ya kupikia.

Chalamila amesema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni kinara wa matumizi ya nishati chafu, hivyo uwamuzi wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania kugawa mitungi hiyo ya gesi itasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusisitiza kuwa kupika kwa gesi ni nafuu ukilinganisha na kuni au mkaa ambao mbele ya safari una madhara Mengi ya kiafya ambayo yatahitaji fedha nyingi kuyatibu.

“Dar es salaam ndio Mkoa unaotumia nishati chafu kutokana na wingi wa watu wanaotumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupika hivyo uamuzi huu wa Puma Energy Tanzania unakwenda kumaliza au kupunguza matumizi ya nishati chafu katika Mkoa wetu na Tanzania kwa ujumla.

Akigusia faida za kutumia nishati safi amesema ni pamoja na Kusaidia kuokoa muda mwingi unaotumika kupika kwa kuni na mkaa, kuokoa gharama na kubwa zaidi ni kuepuka madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah amesema kampuni hiyo imedhamiria kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na ndio wameitoa mitungi hiyo ambayo itagawanywa katika wilaya zote tanı za Mkoa huo.

“Katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna shughuli nyingi miongoni mwa shughuli hizo ni biashara ya chakula
kinachoandaliwa kwa wingi kutoka kwa Mama Lishe ambao wanakumbana na changamoto nyingi, mojawapo ikiwa upatikanaji wa nishati ya kupikia, hususan nishati safi na salama,” ameeleza.

Amesema Puma Energy Tanzania inaelewa serikali chini ya Rais Samia imekuwa na mpango kazi kwa miaka kadhaa wa kuelimisha na kueneza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wote.

Fatma Abdallah, Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania

Amesema Jitihada hizo zimejionyesha katika mikutano ya ndani na nje ya nchi ambayo Rais Samia amekuwa akishiriki kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya nishatisafi unaimarika.

“Tunatambua wajibu wake wa kushiriki katika masuala ya maendeleo ya jamii, hivyo itaendelea kushirikiana na serikali inayoongozwa na Rais Samia kuhakikisha kampeni ya nishati safi inafanikiwa kwani dhamira ya rais ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi na sisi tuko naye kufikia malengo hayo,” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!