January 11, 2025

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Walioua kwa deni la 300,000/- watiwa mbaroni

 

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani, linawashikilia watu wanne kwa tuhuma za mauaji ya Juma Saidi Mfaume (40), mkazi wa Mbagala, Mlandizi kisa deni la shilingi 300,000. Anaripoti Mwandishi Wetu, Pwani … (endelea).

Taarifa za awali zinaeleza kuwa mke wa marehemu Juma, Khadija Ramadhani na mumewe, walikopa kiasi cha shilingi 300,000 kwenye kampuni ya OYA na walishaanza kufanya marejesho ya mkopo huo.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, ACP Muhudhwari Msuya, amesema mauaji hayo yalitokea juzi Jumatatu Oktoba 7, na kwamba tayari jeshi hilo linawashikilia watu wanne.

Alisema watuhumiwa walimpiga Juma kwa kitu kizito kichwani ndipo alipoanguka na kupoteza fahamu, hivyo kulazimika kumbeba kwenye gari lao na kumpeleka Kituo Cha afya cha Mlandizi, ambako alifariki akiwa anapatiwa matibabu.

“Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na daktari kisha kukabidhiwa ndugu kwa taratibu za mazishi. Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani linatoa wito kwa kampuni na taasisi za a kifedha, kufuata taratibu za kisheria katika kudai fedha kutoka kwa wateja wao, ili kuepusha usumbufu na madhara yanayoweza kutoka ikiwamo uharibifu wa mali, kujeruhi na vifo,” alisema.

Akizungumzia mkopo huo, Khadija alisema walikuwa wanarejesha Sh. 34,000 kila wiki na kwamba ilikuwa imebakia Sh. 102,000 kumaliza deni hilo.

Hata hivyo, alisema kabla ya kukamilisha deni hilo, wakopeshaji hao walifika nyumbani kwake na kumkuta mwanamke huyo akiwa peke yake, ndipo walipomshawishi akope tena na kukubali kuingia deni jipya la Sh. 300,000 bila kumwambia mumewe.

Alisema kutokana na usiri wa mkopo huo, alilazimika kufanya marejesho kimya kimya hadi alipopata safari ya kwenda nyumbani kwa Tanga, wiki moja iliyopita.

Khadija alisema akiwa safari, alishindwa kurejesha mkopo kama makubaliano yalivyotaka, ndipo maofisa wa OYA walipoanza kufuatilia hadi walipofika nyumbani kwake.

Akisimulia kwa uchungu, alisema siku ya mzozo baina ya maofisa hao na mumewe, walimkuta nyumbani na kumtaka atoe rejesho, ndipo yakatokea mabishano ambao uliosababisha maofisa kutaka kuingia ndani, huku mumewe akiwazuia.

Imeelezwa kuwa mumewe aliinama kuvaa viatu na hapo ndipo akapigwa na kitu kizito na kudondoka chini.
Aidha, mfanyakazi aliyempiga alipoona Juma amedondoka, alikimbia; na wenzake wakalazimika kumkimbiza hospitali, ambako umauti ulimkuta.

About The Author

error: Content is protected !!