JUMLA ya makatibu 25 wa kamati za huduma ya mikopo ngazi ya kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu pamoja na maofisa maendeleo ya jamii 10 ngazi ya wilaya, wamepatiwa mafunzo ya usimamizi wa mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri huku wakisisitizwa kuzingatia kanuni na mwongozo katika utoaji wa mikopo hiyo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Mafunzo hayo ya siku mbili, yameanza kutolewa jana tarehe 9 Oktoba, 2024 katika ukumbi wa Shule ya Msingi Itumbili mjini Magu mkoani Mwanza kwa lengo la kuwawezesha washiriki hao kuwa wasimamizi pamoja na kuhamasisha vikundi vyote kuhusu utoaji wa mikopo hiyo.
Mkufunzi wa mfunzo hayo ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii anayeratibu mikopo vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika halmashauri ya wilaya ya Magu, Shida Missana amesema katika halmashauri hiyo ya Magu wanatarajia kutoa mikopo ya Sh. 889.9 milioni.
“Mikopo hii ilisimama mwaka jana lakini mwaka huu tumekuwa na muongozo mpya wenye kanuni mpya hivyo tunapitia muongozo pamoja na kanuni zote ili wasimamizi hawa wawe tayari kwa ajili ya kuhamasisha vikundi, kuunda vikundi pamoja na kuwaongoza katika suala zima la kuomba mikopo hii ambayo ni asilimia 10 za mapato zinazotengwa na halmashauri.
“Kwa upande wa Magu tumepata Sh milioni 889.9 na kwa sasa tupo kwenye maandalizi ili kuanzia mwezi Novemba mwaka huu tuanze kutoa mikopo,” amesema.
Amewaasa wasimamizi hao kuhakikisha mikopo hiyo inatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali au vikundi vyenye mawazo ya kijasiriamali ili kuwezesha makundi yaliyolengwa kujikwamua kiuchumi.
Amesisitiza kuwa makundi ya watu wenye ulemavu yanatakiwa kuwa na watu kuanzia wawili kuendelea huku makundi ya vijana na wanawake wakitakiwa kuwa na watu wasiopungua watano.
“Maombi ya mikopo hii inatakiwa kuwa imechakatwa na kukamilika ndani ya miezi miwili,” amesema, Missana.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ya siku mbili, Abubakari Msere ambaye pia ni afisa maendeleo ya jamii katika halamshauri hiyo, aliushukuru uongozi wa halmashauri hiyo kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo amesema yatakuwa chachu kwao katika usimamizi dhabiti wa mchakato mzima wa utoaji wa mikopo hiyo na kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza.
ZINAZOFANANA
Ujenzi wa barabara, madaraja Babati kufungua Utalii
Mradi wa Nishati Safi wa EWURA kupunguza madhara ya kuni kwa jamii
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA Dar