MKUU wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Joshua Nassari amewataka wenyeviti na vitongoji na vijiji katika wilaya hiyo kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa unafanyika kwa amani, utulivu na kudumisha umoja kwa masilahi mapana ya Taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mwanza … (endelea).
Mkuu wa wilaya hiyo ametoa wito huo jana tarehe 3 Oktoba 2024 mjini Magu wakati akizungumza na wenyeviti hao kutoka vijiji 82 na vitongoji 508 vya wilaya hiyo.
Amesema asili ya uchaguzi ni sawa na vita ambayo kila upande huvutia upande wake, lakini kwa vilevile wenyeviti hao ambao wanamaliza muda wao nao watagombea, pindi ikitokea wameshindwa wakubali matokeo badala ya kuibua makundi yasiyokuwa na msingi ndani ya wilaya hiyo.
“Unapofika wakati wa uchaguzi ni sawa na vita, hivyo hata katika nafasi ya ubunge, mbunge wetu (Boniventura Kiswaga) inapotokea mtu amechukua fomu kuwania nafasi yako katika uchaguzi mkuu wa mwakani, usikasirike kwa sababu watu wanaona kazi kubwa uliyoifanya,” amesema.
Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu, Nassari amewaahidi wenyeviti hao kuwa licha ya uongozi wao kutarajiwa uvunjwa Oktoba 25 mwaka huu kuelekea kwenye uchaguzi huo, hakuna jasho la mwenyekiti yeyote litakalopotea.
Aidha, akizungumza katika mkutano huo, Mbunge wa jimbo hilo, Boniventura Kiswaga (CCM) aliwapongeza wenyeviti hao kwa kuwa kielelezo bora cha kuleta maendeleo kwa wananchi hasa ikizingatiwa wao ndio wasimamizi wa miradi inayoelekezwa na serikali kwenye maeneo yao.
Pia amewaonya wenyeviti hao ambao wengine watatetea nafasi zao, kuzingatia kuwa matokeo ya uchaguzi huo yatatokana na namna walivyokuwa wamejenga mahusiano mazuri na wananchi na sio utekelezaji wa miradi ya maendeleo pekee.
“Lakini pia mnaweza kujitetea kwa sababu kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan hakuna kijiji ambacho hakijaguswa na miradi ya maendeleo, kuanzia maji, ujenzi wa zahanati na hata barabara,” amesema.
Amesema asilimia 98 ya wenyeviti hao wanaweza kutetea nafasi zao iwapo watajieleza vizuri kwa wananchi hivyo ni lazima kusimama na kushinda uchaguzi huo kwa heshima.
Naye Afisa Uchaguzi wilaya ya Magu, Mwagala Masunga amesema zoezi la kuandikisha wapiga kura uchaguzi huo litaanza tarehe 11 hadi 20 Oktoba mwaka huu huku kampeni zikitarajiwa kuanza tarehe 20 hadi 26 Novemba mwaka huu.
“Tunatarajia zaidi ya wananchi 215,000 wataandikishwa na kuwa na sifa za kupiga kura katika uchaguzi huu, msisitizo ni kwamba kila mtu ajiandikishe kwenye kitongoji chake,” amesema.
ZINAZOFANANA
Ujenzi wa barabara, madaraja Babati kufungua Utalii
Mradi wa Nishati Safi wa EWURA kupunguza madhara ya kuni kwa jamii
TCC yaibuka kidedea tuzo za PMAYA Dar