October 17, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

TEF yataka mazungumzo ya serikali, Mwananchi Communications

 

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limeishauri serikali na kampuni ya Mwananchi Communications, wakae meza moja, ili kufungua leseni za maudhui mtandaoni, ziliyositishwa kwa siku 30 kuanzia jana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, katika taarifa aliyoitoa leo Alhamisi kwa vyombo vya habari, amesema meza ya mazungumzo ndiyo itakayomaliza changamoto iliyojitokeza; na kwamba hilo lifanyike kwa maslahi ya taifa na uhuru wa vyombo vya habari nchini.

“Kwa vyovyote vile, tayari tatizo limetokea na kinachotakiwa sasa tunashauri pande zote mbili; Serikali na Mwananchi Communications, wakutane na kujadili suala hili na kulimaliza kwa masilahi mapana ya taifa na uhuru wa vyombo vya habari ndani ya muda mfupi kadri inavyowezekana,” amesema Balile.

Amesema TEF bado inadai chombo huru kwa ajili ya kusikiliza na kutoa uamuzi, pale vyombo vya habari vinapotuhumiwa kukiuka masharti ya leseni.

“Kwa muda mrefu TEF, tumekuwa tukilalamikia mamlaka makubwa yanayotolewa kisheria, kwenye taasisi au wakuu wa taasisi ya kuwa walalamikaji, waendesha mashitaka na watoa hukumu, bila upande wa pili unaotuhumiwa kupewa fursa ya kusikilizwa.”

“Tutaendelea kudai haki hii ya asili (natural justice), ya chombo cha habari kinachotuhumiwa kupewa hati ya mashitaka, kikajitetea mbele ya taasisi huru au Mahakama, kisha uamuzi ufanyike ambao ndiyo utawala wa sheria, badala ya sasa ambapo sheria inatoa mamlaka kwa mtu mmoja kufanya uamuzi mzito kama huu,” amesema Balile.

Amesema Mwananchi walipaswa kufunguliwa mashataka katika chombo huru na wao kujitetea, kisha chombo hicho kikatoa hukumu, kulingana na mashtaka na utetezi uliowasilishwa mbele yake.

“Tumeviona pia vibonzo au maudhui yaliyolalamikiwa na TCRA. Tunawasihi wahariri na watendaji wa vyombo vya habari kufahamu kuwa, sheria mbaya inaendelea kuwa sheria hadi itakapobadilishwa…tunawasihi wahariri na waandishi nchini kufahamu ukweli, kuwa utamaduni unatofautiana nchi hadi nchi,” amesema

Amesema vyombo vya habari vitumie njia za kufikisha ujumbe kwa njia sahihi badala ya kujiingiza katika mazingira yanayoweza kutafsiriwa kama kejeli.

Jana tarehe 02 Oktoba 2024, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabiri Bakari, alitangaza kusitisha leseni za huduma za maudhui mtandaoni za kampuni ya Mwananchi Communications Limited (The Citizen, Mwananchi Digital, Mwananchi na MwanaSpoti), kwa siku 30.

TCRA imesitisha leseni hizo, kwa madai kuwa mitandao ya Mwananchi Communications, ilichapisha maudhui yaliyokiuka kanuni, ambayo yameleta tafsiri hasi kwa taifa, jambo ambalo linaathiri na kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa.

About The Author