October 1, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Masauni ataka magereza kuchangamkia kilimo

 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni, amehimiza maboresho ya kimfumo, kimuundo na kitaasisi katika Jeshi la Magereza nchini, ili kuliongezea uwezo wa uzalishaji wa mazao ya kilimo, ambayo yana soko la uhakika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Ruvuma … (endelea).

Waziri Masauni amesayasema hayo tarehe 30 Septemba 30, 2024 wakati wa ziara yake katika Gereza la Kilimo na Mifugo Kitai lililoko Mbinga, mkoani Ruvuma.

Amesema maboresho yatatenganisha mamlaka ya kiutawala ya Jeshi la Magereza na Shirika la Uzalishaji Mali la jeshi hilo (SHIMA), ili kurahisisha usimamizi wa shughuli za kibiashara.

Amelielekeza jeshi hilo kuchangamkia fursa za kilimo cha nafaka kwa kupanua maeneo ya mashamba, kutokana na fursa ya soko la Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA).

“Serikali imetangaza bei nzuri ya ununuzi wa mazao, lakini bado hakuna jitihada kutoka Jeshi la Magereza kuchangamkia fursa hii,” amesema.

Aidha, amehimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia, akitaka kuachana na kuni na mkaa, ili kulinda mazingira.

Kwa upande wake, mkuu wa gereza la kilimo na mifugo Kitai, SP Gabriel Luderi, amesema gereza hilo lipo tayari kwa mabadiliko yanayolenga kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuboresha utendaji wake wa kazi.

*Mwisho.*

About The Author