FAMILIA ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, Edward Sokoine, imesema imetamani kuandika kitabu cha historia ya kiongozi huyo kwa zaidi ya miaka 30. Anaripoti Restuta James, Dar es Salaam … (endelea).
Mtoto wa kiongozi huyo, Balozi Joseph Sokoine, ameyasema hayo leo kwenye hafla ya uzinduzi wa kitabu cha hayati Sokoine: Maisha na Uongozi, inayofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, ni mgeni rasmi.
“Leo ni siku muhimu kwa familia na naamini kwa Watanzania wote, hatimaye ndoto ya karibia miaka 40 ya kusoma kitabu cha maisha na uongozi cha mmoja wa viongozi wetu imetimia kwa msaada wako,” amesema Balozi Sokoine.
Amesema kiu yao ilipata mwanga Machi 2021, alipopigiwa simu na msaidizi wa Makamu wa Rais, kuomba kitabu au maandishi yanayomhusu Sokoine.
“Nilimjulisha kuwa nilikuwa nina kitabu cha hotuba ya mzee aliyokuwa ameitoa Machi 1983 na nikamweleza kuwa kuna hotuba nyingine aliyokuwa ameitoa Oktoba 1982 kwenye mkutano mkuu wa chama. Niliahidi kumtumia kitabu hicho na nilifanya hivyo,” amesema.
Amesema baada ya muda mfupi, alipokea simu nyingine iliyomuunganisha moja kwa moja na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, ambaye aliongea nae kwa kirefu kutaka kujua kama familia ina kitu kingine kilichowahi kuandikwa kuhusu hayati Sokoine.
“Nimweleza kuwa kulikuwa na kitabu kimoja ambacho kilikuwa kimeandikwa mwaka 1984 au 1985, ambacho kilielezea maisha ya mzee kidogo na kilikuwa na hotuba zake alizokuwa amezitoa bungeni.
Nilitumia fursa hiyo kumweleza Makamu wa Rais juu ya juhudi ya familia ya zaidi ya miaka 30 ya kutaka kuandika kitabu juu ya mzee bila mafanikio.”
“Baada ya maelezo yangu, alinieleza umuhimu wa kuandikwa kwa vitabu vya viongozi na watu mashuhuri ili tusipoteze urithi na sehemu ya historia ya nchi yetu,” amesema Balozi Sokoine.
Edward Moringe Sokoine, alizaliwa tarehe 1 Agosti 1938 na kufariki kwa ajali tarehe 12 Aprili 1984, akiwa na umri wa miaka 45.
Aliwahi kuwa Waziri Mkuu mara mbili, tangu tarehe 13 Februari 1977 hadi 7 Novemba 1980; na tarehe 24 Februari 1983 hadi umauti ulipomkuta mkoani Morogoro, akitokea Dodoma.
Sokoine anakumbukwa kwa jinsi alivyokuwa na uadilifu na kufuatilia utendaji kazi, huku akikemea rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.
Alikuwa Mkristo wa Kanisa Katoliki, akiwa mwanachama wa Utawa wa Mtakatifu Fransisko.
ZINAZOFANANA
Polisi wadai Chadema wamewapiga mawe
Serikali yaipa ITA jukumu la utafiti wa mapato
Mbowe, Sugu wakamatwa na Polisi mkoani Songwe