KUNDI la wanamgambo la Hezbollah la nchini Lebanon, limethibitisha kuuawa kwa kiongozi na mmoja wa waanzilishi wake, Hassan Nasrallah, katika shambulizi la anga la Israel jana, Septemba 27. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Hezbollah, Sayyed Hassan Nasrallah, imesema pamoja na kifo hicho, kundi hilo litaendeleza ‘vita vyake vitakatifu’ dhidi ya Israel na katika kuiunga mkono Palestina.
Taarifa hiyo inathibitisha kile kilichoelezwa awali na jeshi la Israel, lililosema Hassan Nasrallah, aliuawa katika shambulizi ‘sahihi’ la anga wakati wa mkutano wa viongozi wa kundi hilo kwenye makao yake makuu mjini Dahiyeh, kusini mwa Beirut, nchini Lebanon.
Imedaiwa kwamba mawasiliano ya Nasrallah yalipotea tangu siku ya Ijumaa, wakati shambulizi lilipofanyika.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi la Israel, Luteni Kanali Shoshani, amesema bado wana kazi kubwa ya kufanya na mapigano dhidi ya kundi la Hezbollah yanaendelea.
“Hezbollah bado wana roketi na makombora na kundi hilo lina uwezo wa kuyarusha makombora mengi kwa wakati mmoja,” alifafanua msemaji huyo wa jeshi la Israel.
Katika mashambulizi ya mfululizo yaliyoanza mapema wiki hii, jeshi la Israel (IDF), limeshambulia maeneo 140 ya Hezbollah ikiwamo mizinga, majengo ya kuhifadhi silaha, silaha za kimkakati, viwanda vya kutengeneza silaha na miundombinu mingine ya kundi hilo, likidai ni ngome za kigaidi.
Naye mkuu wa majeshi ya Israel, Luteni Jenerali Herzi Halevi, amesema Israel itaendeleza mashambulizi yake dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran, hata baada ya mauaji ya Nasrallah.
“Kuuawa kwa Nasrallah sio mwisho wa mashambulizi yetu,” alifafanua Luteni Jenerali Halevi.
Katika taarifa iliyoshirikishwa kwenye akaunti ya mtandao wa X ya IDF, inasema: “Hassan Nasrallah hataweza tena kutishia ulimwengu.”
Katika taarifa hiyo, Israel imesema kwamba wanachama wengine waandamizi wa kundi linaloungwa mkono na Iran, waliuawa pamoja na Hassan Nasrallah – ikiwa ni pamoja na kamanda wa eneo la kusini la Hezbollah.
IDF inasema ndege za kivita zilifanya “shambulizi lililolengwa” katika makao makuu ya kati ya Hezbollah, ambayo inasema yapo “chini ya ardhi ya jengo la makazi katika eneo la Dahieh huko Beirut”.
Katika hatua nyingine, kundi la Hezbollah limesema linahusika na mashambulizi kadhaa ya makombora dhidi ya Israel. Kwa mujibu wa Hezbollah, kundi la wanajeshi wa Israel walishambuliwa kwa mizinga kaskazini mwa Israel.
Hezbollah imesema roketi lilirushwa kuelekea Kibbutz Sa’ar, na kwamba makombora zaidi yalirushwa katika kijiji cha Rosh Pina, ikiwa ni katika kulipiza kisasi, mashambulizi ya Israel nchini Lebanon.
Naye Kiongozi Mkuu wa kidini na mwenye mamlaka makubwa zaidi nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amelaani vikali kile alichokitaja kuwa sera ya ‘kipumbavu na kijinga’ ya utawala wa Israel baada ya mashambulizi yake nchini Lebanon.
Khamenei amesema mauaji ya watu wasio na ulinzi nchini yanafichua ukatili wa Israel.
”Hatma ya ukanda huu itaamuliwa na vikosi vya upinzani, huku Hezbollah ikiwa mstari wa mbele,” alisisitiza Khamenei katika taarifa yake aliyoitoa leo Jumamosi.
Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya (EU), umeyashauri mashirika ya ndege kuepuka kutumia anga ya Lebanon na Israel kwa mwezi ujao, huku kukiwa na ongezeko la mashambulizi ya anga kati ya Israel na Hezbollah.
Taarifa ya Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya na Shirika la Usalama wa Anga la Umoja wa Ulaya (EASA), iliyotolewa leo imeonya kwamba kuna wasiwasi wa kuongezeka kwa mashambulizi ya anga na kuzorota kwa hali ya usalama.
EASA imesema itaendelea kufuatilia kwa karibu hali katika eneo hilo, kwa nia ya kutathmini kama kuna ongezeko au kupungua kwa hatari kwa mashirika ya ndege ya Umoja wa Ulaya, kutokana na kitisho kinachoendelea.
ZINAZOFANANA
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani
Ushindi wa Profesa Lipumba wapingwa
Ukraine wakiri kufanya mauaji ya Jenerali wa Urusi na msaidizi wake mjini Moscow