December 25, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Dk. Biteko aliomba kanisa ulinzi wa amani

 

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amelitaka kanisa kulinda amani nchini, huku akiwahimiza viongozi wa dini kusimamia misingi ya malezi na makuzi ya kwa watoto, ili kudumisha tunu hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Dk. Biteko amesema hayo leo tarehe 26 Septemba 2024, jijini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa Kanisa la Pentecostal Assemblies of God, Tanzania (PAG).

Amesema malezi na makuzi ndiyo yatakayosaidia kulinda na kuhifadhi tunu ya amani nchini, akieleza kuwa Kanisa lina nafasi ya kulinda amani iliyopo na kwamba viongozi wa dini wasikubali tofauti za kibinadamu kuivuruga.

“Kuna watu ni wakandarasi wa uongo na wengine ni mawakala wa uongo. PAG tukawafundishe watu kuwa uongo wa aina hiyo unaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuna watu wangependa tofauti zetu za dini, kabila na mitazamo yetu, igeuzwe mtaji wa kisiasa, tusikubali na tuendelee kuwa wamoja na kuilinda tunu ya amani yetu,” amesema.

Dk. Biteko amesisitiza pia umuhimu wa kuzilinda mila nzuri na kujiepusha na tamaduni zinazosababisha mmomonyoko wa maadili.

Awali, Askofu Mkuu wa PAG (Tanzania), Dk. Daniel Awet, aliiomba Serikali kuweka mazingira rafiki kwa Watanzania ili kuimarisha demokrasia, haki na misingi ya amani.

Amemwomba Dk. Biteko afikishe salamu za Kanisa hilo kwa Rais Samia Suluhu Hassan, akimweleza kuwa waumini wanatambua kazi kubwa na nzuri inayofanywa na Serikali anayoingoza.

About The Author

error: Content is protected !!