October 13, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

EACOP kutoa fursa za   ajira kwa vijana 143 wa Tanzania, Uganda

 

MRADI wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) utatoa ajira kwa vijana wazawa 143 kutoka nchini Tanzania na Uganda waliofuzu mafunzo ya kozi maalum ya nishati za gesi na mafuta  iliyoendeshwa kwa njia ya mtandao ‘Massive Open Online’ (MOOC) ili kupata ajira katika mradi huo unaoanzia Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mafunzo hayo mkoani Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa EACOP Bw. Guillaume Dulout alisema  lengo la mafunzo hayo ni   kuwajengea uwezo vijana wazawa  kwa kuwapa maarifa yatakayotoa mchango  stahiki  katika kukuza sekta ya mafuta na gesi sambamba na  kuwanufaisha wananchi wa  Tanzania na Uganda wanaopitiwa na mradi huu.

Takriban vijana 2,000 walijiandikisha, huku 143 wakifaulu na kupata ajira katika awamu hii.

“Ili kuwapa vijana wazawa wa nchi hizi mbili (Tanzania na Uganda), ujuzi na maarifa kuhusu sekta ya gesi na mafuta, tumeamua kutoa mafunzo haya ili kutoa ujuzi na maarifa kwa jamii zinazopitiwa na mradi huu ili kuja kuwa na wataalamu watakaotumika katika miradi mingine pindi mradi huu utakapoisha,” alisema Dulout.

Kwa upande wake  Meneja mafunzo kutoka EACOP, Laurent Stephane, alisema mafunzo hayo  ni ishara ya wazi katika  kuchochea  maendeleo endelevu katika sekta ya mafuta na gesi baina ya nchi hizo mbili  sambamba na kuwa na vijana  wataalamu  ambao ni wazawa.

“EACOP inaendelea kutilia mkazo maendeleo ya vipaji vya wazawa na imejipanga kukuza ukuaji wa uchumi na uendelevu katika ukanda huu.

“Uzinduzi wa mafunzo haya ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba manufaa ya sekta ya mafuta na gesi yanashirikishwa kwa upana, hasa miongoni mwa vijana ambao ni nguzo ya mustakabali wa mataifa haya,” alisema Stephane.

Naye Mratibu wa mradi huu kwa upande wa Tanzania kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Asiadi Mruto alisema  ujenzi wa mradi huu kwa sasa umefikia asilimia 43.5% ambapo miundombinu ya ujenzi inaendelea kwa upande wa Tanzania na Uganda.

“Mafunzo haya yataanza  kwa awamu tofauti awamu ya kwanza, wanafunzi watajifunza kwa miezi miwili  katika chuo cha ufundi  Arusha (ATC)  na  baadaye  watapelekwa  kwenye chuo cha Elimu ya Ufundi Stadi (VETA) Moshi  ambapo watajifunza kwa muda wa miezi mitatu baada ya hapo  watapelekwa nchini Uganda kwenye chuo cha  Uganda Petroleum Institute Kigumba (UPIC)  ambapo pia watapata mafunzo kwa muda wa miezi sita   na mwisho  wataenda nchini  Ufaransa  kumalizia mafunzo yao ambayo yataangazia  zaidi mradi wa EACOP,” alisema Mruto.

Katika hatua nyingine, Mruto amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu hassan imejidhatiti katika kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafikia malengo yaliyowekwa.

Naye Mkurugenzi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kanda ya Kaskazini, Monica Mbele alisema   chuo cha Veta Moshi pia kitatumika kutoa mafunzo kwa vijana hao 143.

“Tumefaidika sana kwa ujio wa  mradi huu  kwani walimu wetu wameweza kupata mafunzo mbalimbali kutoka kwa wataalamu  wabobezi kutoka  makampuni za kimataifa,” alisema Mbele.

Alisema EACOP imeendelea kufanya maboresho katika chuo hicho,  ambapo tayari wameshatoa fedha kwa ajiri ya ukarabati wa majengo  ikiwemo mabweni na madarasa  sambamba na vifaa vya kisasa  vya kufundishia  kulingana na fani zitakazotolewa hivyo mashirikiano hayo yamekuwa na tija  si kwa wanafundi na walimu pekee bali  kwa chuo kizima.

Oikitoki Lumenyo ambaye ni mnufaika wa mafunzo hayo alisema kupitia elimu anayopata itamsaidia kwenda kuwaelimisha jamii yake ya kimasai   faida za mradi huo ikiwemo   kufanya kazi kimataifa kwenye miradi mikubwa yakimkakati.

Wana hisa wa mradi wa EACOP ni Total Energies ikimiliki asilimia 62, Mashirika ya kusimamia mafuta nchini Tanzania (TPDC) na UNOC ya Uganda yakimiliki asilimia 15 kila moja, wakati shirika la mafuta nchini China (CNOOC) linamiliki asilimia nane tu.

About The Author