November 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Afande ‘aliyelipa’ wabakaji afikishwa mahakamani

 

HATIMAYE Fatma Kigondo, Afisa wa Jeshi la Polisi, anayetuhumiwa kuwa ndiye “Afande” aliyetajwa na kundi hilo la vijana, lililomfanyia vitendo vya kikatili msichana mmoja, aliyepachikwa jina la “Binti wa Yombo,” amefikishwa mahakamani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mtuhumiwa alifika kwenye Mahakama ya Dodoma, leo Alhamisi, huku akiwa amejifunika gubigubi na hivyo kuwapa wakati mgumu wandishi wa habari kutambua aliingia muda gani mahakamani hapo.

Hata hivyo, shauri dhidi ya afisa huyo, limeahirishwa hadi tarehe 7 Oktoba mwaka huu, kutokana na hakimu Francis Kisenyi aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, kuhamishwa kituo cha kazi.

Awali shauri hilo lilipangwa kwa mara ya kwanza 23 Agosti, mbele ya hakimu mkazi wa Mahakama ya mkoa wa Dodoma, Francis Kishenyi. Lakini Afande Fatma hakufika mahakamani na kusababisha shauri kuahirishwa hadi leo tarehe 5 Septemba.

Akizungumza nje ya mahakama hiyo, Paul Kisabo, mmoja wa mawakiili waliyofungua kesi hiyo alisema, “Tumepewa taarifa kwamba, hakimu amehamishwa. Kwa hiyo, shauri lilipangwa kuhairishwa mbele ya muheshimiwa Tungalaja ambaye mamlaka yake katika shauri hili, ni kuahirisha tu kwa sababu shauri halijapangiwa hakimu.”

Aliongeza, “lakini tunashukuru mshitakiwa, Fatma Kigondo, amefika mahakamani. Shauri limeahirishwa hadi tarehe 7 Oktoba. Tunaamini siku hiyo tutakuta shauri limepangiwa hakimu kwa ajili ya kusikiliza na kama itakuwa imeishapangiwa tayari, maana yake usikilizaji wa kesi hii utaanza mara moja.”

Hatua hiyo ya hakimu wa shauri hilo la Afande anayetuhumiwa kufadhili tukio la ubakaji na ulawiti kwa binti wa Yombo Dovya jijini Dar es Salaam kupangiwa kituo kingine cha kazi, limeibua hasira kutoka kwa makundi mbalimbali wakiwemo wanaharakati wa kutetea haki za binadamu.

Charles Odero, afisa kutoka asasi ya msaada wa kisheria, jijini Arusha anasema, “…kama kweli Mahakama ilijua kwamba kesi hii ina umuhimu wake, kwanini imemuhamisha aliyepangiwa kuisikiliza?”

Anaongeza: “Kwa kweli, inasikitisha sana kwamba Mahakama inazidi kujiondolea uhalali wake kwa wananchi. Uhalali wa Mahakama utabaki kwenye makaratasi ya sheria tu. Wananchi watazidi kuidharau Mahakama.”

Tayari washitakiwa wanne wamefunguliwa kesi ya ubakaji kwa kundi na kuingilia kinyume na maumbile binti huyo na iko mbele ya hakimu mkuu mkazi, mkoa wa Dodoma, Zabibu Mpangule.

About The Author