WASOMI na wataalamu mbalimbali nchini wameelezea kuvutiwa kwao na utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika ya Mashariki (EACOP) wakisema umekidhi vigezo vyote vinavyotakiwa kimataifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Morogoro … (endelea).
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wasomi hao wamesema utekelezaji mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga mbali ya kukidhi vigezo vyote utachagiza maendeleo ya haraka kwa jamii zilizopitiwa na mradi.
Aliyekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na hatimaye Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Profesa Faustin Kamuzora amepongeza mradi huo na kusema umekuwa na matokeo chanya katika maeneo yote uliopita.
“Huu mradi ni mkubwa na umezingatia taratibu zote za kimazingira na ubora wake ni hali ya juu. Mimi ni mwenyeji wa Kagera na nimefanya kazi kama Katibu Tawala wa mkoa huo ambako mradi umeanzia ukitokea Uganda,” amesema Prof Kamuzora ambaye pia ni Mhadhili wa Chuo Kikuu cha Sokoine.
Prof Kamuzora alisema miongoni mwa miradi ambayo ameshawahi kuiona na utekelezaji wake ukiwa wa viwango vya hali ya juu ni wa EACOP kwani mbali ya kukidhi viwango vya kimataifa,umekuwa ni manufaa pia kwa wananchi.
“Mradi wa EACOP nimeufuatilia tangu upembuzi yakinifu unaaanza yaani ‘feasibility study’ yake mpaka hatua hii ya utekelezaji wake,” alisema na kuongeza kuwa mradi utabadilisha sana maisha ya watu.
Dk. Tasco Romanus Luambano, Wakili Msomi na Mhadhili Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe katika Kampasi ya Mbeya amesema mradi EACOP ni miongoni mwa mradi inayoiweka Tanzania katika ramani ya dunia.
“Nazipongeza sana serikali za Uganda na Tanzania kukubaliana mradi upite kwenye ardhi ya nchi hizi mbili. Ni mradi ambao ukamilikaji wake utabadilisha maisha kwenye maeneo mradi umepita katika mkoa ile minane,” amesema Dkt Luambano.
Naye Mtaalamu wa Oil na Gesi, Bw Jackson Jalimba amezipongeza serikali za Tanzania na Uganda kwa kukubaliana utekelezaji wa mradi huo kwani una manufaa yake ya kiuchumi na kijamii ni makubwa sana.
Bomba hili linapita katika mikoa nane ya Tanzania Bara ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga, likijumuisha wilaya 24, kata 134 na vijiji zaidi ya 180.
Wanahisa wa mradi huu ni TotalEnergies (Asilimia 62), kampuni ya mafuta ya Uganda (UNOC) asilimia 15, CNOOC ya China asiimia nane pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) asilimia 15.
ZINAZOFANANA
Polisi: Waharifu 2024 wapungua mkoani Songwe
Jeshi la Polisi: Sherekeheni sikukuu kwa utulivu na amani
Mil.600 zatengwa kupeleka umeme Kijiji cha Ijinga – Magu