October 16, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Dk. Mpango aagiza TARURA kukarabati barabara Kondoa

 

Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango ameagiza Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA) kufanya ukarabati wa Barabara ya Ntundwa – Hurui ya Wilayani Kondoa ili kuwarahisishisa wananchi shughuli za kiuchumi ikiwemo usafirishaji mazao. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Makamu wa Rais ametoa maagizo hayo leo Jumatano baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Daraja la mto Hurui lililopo kata ya Kikore Wilaya ya Mpwapwa akiwa ziarani mkoani Dodoma.

Amewahimiza wananchi wa kata ya Kikore na watumiaji wa daraja hilo kutunza miundombinu iliyojengwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye.

Pia amewaagiza kupanda miti maeneo yote pemebezoni mwa mto Hurui ili kuokoa daraja hilo lisiharibike kutokana na mmomonyoko wa udongo.

Nawapongeza wananchi hao kwa kupata mradi wa daraja uliowaondolea changamoto waliyopata ya kukosa daraja tangu mwaka 2019 lilipoharibiwa na maji daraja la awali lakini pia niwahakikishie kuwa serikali itaendelea kuwafikishia huduma muhimu ikiwemo miundombinu,” amesema.

Makamu wa Rais akiwa katika kata ya Kikore ameagiza kukamilishwa kwa mradi wa maji unaotekelezwa katika kata hiyo ifikapo tarehe 30 mwezi Oktoba 2024.

Aidha, ameiagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Mbunge wa Kondoa Vijijini kushughulikia changamoto iliyotolewa na wananchi wa Kijiji cha Hurui kuhusu ardhi ya Kijiji inayodaiwa kuuzwa kwa mwekezaji bila kufuata utaratibu.

Ujenzi wa Daraja la Hurui umegharimu Sh 1.6 bilioni na linatarajiwa kuwa kiungo muhimu na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa kurejesha mawasiliano kati ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma na Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Daraja hilo lenye urefu wa Mita 30 limejengwa kwenye barabara ya Ntundwa – Mkunduru -Hurui yenye urefu wa kilometa 46.4.

Mradi huo umehusisha uboreshaji wa kilometa 8 za barabara kwa kiwango cha changarawe na umegharamiwa na Serikali kupitia tozo ya mafuta ya shilingi 100.

About The Author