IMEELEZWA kuwa wanaume wanaongoza kwa maambukizi ya ugonjwa wa homa ya nyani (M-Pox) huku wengi wao wakiambukizwa kupitia ngono. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa… (endelea).
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kwa kila visa 10 vilivyoripotiwa kuhusu Mpox, tisa vinajumuisha wanaume, idadi kubwa wakiwa wameambukizwa kupitia kujamiiana.
Miongoni mwa jumla ya visa 90,140 vya maambukizi, wanaume wanaongoza kwa 87,189, ambapo asilimia 96 waliambukizwa virusi hivyo kupitia kujamiiana.
Katika ripoti ya Shirika hilo iliyotolewa jana Jumatano, imeeeleza kuwa ugonjwa huo umeripotiwa kuathiri zaidi wanaume wenye umri wa miaka kati ya 29-41.
Mgusano kupitia ngono ndiyo njia iliyoripotiwa zaidi kuhusu maambukizi ya homa ya nyani kote duniani huku ikichangia visa 19,102 miongoni mwa 22,801.
“Mtindo huu umeendelea kwa miezi sita iliyopita huku asilimia 97 ya visa vipya ikiripoti mwingiliano wa kingono. Miongoni mwa visa hivyo, dalili zilizojitokeza zaidi ni upele kwenye sehemu nyeti, homa na vipele,” ilisema WHO.
Shirika hilo limesema maambukizi ya homa ya nyani yalifanyika kupitia kujamiiana kwa kutumia mdomo au sehemu nyeti na watu walioambukizwa.
Watu walio na wapenzi wengi, au wapya katika mapenzi, wanakabiliwa na hatari kubwa ya kuambukizwa ugonjwa huo.
“Mtu yeyote aliye na vipele vipya visivyo vya kawaida anastahili kujiepusha kushiriki ngono au kugusana kwa karibu na watu wengine hadi atakapofanyiwa vipimo kuhusu maradhi ya zinaa (STIs) na M-Pox.
“Kumbuka upele huo unaweza pia kupatikana sehemu zisizo rahisi kuona mwilini ikiwemo sehemu nyeti.”
Takwimu zilizokusanywa kutoka kwa mamlaka za kimataifa kufikia tarehe 30 Juni 2024, inaeleza, “Maambukizi kupitia ngono yamerekodiwa vilevile katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) miongoni mwa wachuuzi wa ngono na mashoga.
Tofauti na dalili ya vipele ambayo kwa kawaida inahusishwa na virusi vya M-Pox, baadhi ya watu nchini DRC walionyesha makovu tu kwenye viungo vyao vya uzazi.
Ili kupunguza maambukizi, WHO inapendekeza matumizi ya mipira ya kondomu kila wakati unaposhiriki ngono na kujiepusha na ngono inayojumuisha watu kadhaa kwa pamoja.
WHO vilevile inashauri watu wanaougua M-Pox watumie kondomu wakati wa kujamiiana kwa wiki 12 baada ya kupona.
Aidha, unashauriwa kujiepusha kujamiiana kwenye vituo kama vile vilabu, sehemu za kuvinjari na kunyoosha viungo, ikiwemo kujiepusha kutumia pombe na mihadarati katika mazingira ya ngono.
Aidha, WHO inapendekeza kufunguka mpenzi wako na kuzungumza wazi kuhusu dalili na tishio la homa ya nyani ikiwemo kuwajuza wapenzi kuhusu dalili zozote ulizo nazo, kujiepusha kujamiiana na kupunguza idadi ya wapenzi na kushiriki ngono kiholela.
“Ingawa virusi vya M-Pox vimepatikana kwenye manii, haijulikani kwa sasa ikiwa vinaweza kusambazwa kupitia majimaji ya manii au ukeni,” inafafanua WHO.
“Kuvaa kondumu hakutakukinga kikamilifu dhidi ya M-Pox lakini huenda kukapunguza tishio au kiwango cha maambukizi na kutakusaidia kujikinga dhidi ya HIV na aina nyinginezo za maradhi ya zinaa.”
ZINAZOFANANA
JKCI/ Paul Makonda waandaa kambi ya matibabu ya moyo Arusha
Waziri wa afya aipongeza Shifaa kwa kuanzisha kituo cha tiba na utafiti wa saratani
Mtanzania abainika kuambukizwa Mpox