December 26, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Polisi watii agizo la CCM, Mbowe, wenzake 520 waachiwa kwa dhamana

 

Jeshi la Polisi limekiri kuwakamata na kuwahoji viongozi wakuu wa Chadema pamoja na wafuasi 520 huku baadhi yao akiwamo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wakiachiwa kwa dhamana. Anaripoti Mwandishi Wetu, Mbeya … (endelea).

Viongozi wengine waliokamatiwa mkoani Mbeya eneo la Kadege ni Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, Tundu Lissu; Katibu Mkuu, John Mnyika; Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’; Katibu Mwenezi BAVICHA Taifa, Twaha Mwaipaya na Makamu Mwenyekiti BAVICHA Taifa, Moza Ally.

Jeshi hilo limesema watuhumiwa waliokamatwa katika mikoa mingine pia wamehojiwa na kuachiwa kwa dhamama kisha kurejeshwa walikotoka chini ya usimamizi wa polisi.

Hayo yanajiri saa chache baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emanuel Nchimbi kumuagiza Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamadi Masauni kuwaachia viongozi hao wa Chadema kwani mambo mengine yanahitaji kuzungumzwa kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatatu usiku, Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo, CP – Awadh Haji amesema watuhumiwa hao wamekamatwa kutokana na kukaidi katazo la kupiga marufuku kongamano la vijana wa CHADEMA lililokuwa limepangwa kufanyika katika uwanja wa Ruanda Nzovwe Jijini Mbeya jana Jumatatu tarehe 12 Agosti 2024 kwa mwamvuli wa kuadhimisha siku ya vijana duniani.

Amesema kufuatia katazo hilo, kwa siku ya juzi Jumapili Jeshi la Polisi liliwakamata viongozi na wafuasiwa CHADEMA 375 kati yao wanaume 261 nawanawake 114, ambao walikaidi na kuendelea kufanya safari kutoka mikoa mingine kwa lengo la kutaka kuingia mkoa wa Mbeya kupitia njia mbalimbali ili kutimiza azma hiyo ovu ya kufanya kongamano lililopigwa marufuku.

Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo, CP – Awadh Haji

“Waliokamatwa wakiwa njiani kwenda Mkoa wa Mbeya ni kwamba katika mkoa wa Morogoro walikuwa 28, Mkoa wa Iringa walikuwa 109, Mkoa wa Njombe walikuwa 60, Mkoa wa Dar es Salaam walikuwa 19, Mkoa wa Pwani walikuwa 41, Mkoa wa Rukwa walikuwa 30 na Mkoa wa Songwe walikuwa 51,” amesema.

Amesema tarehe 12 Agosti 2024 Jeshi la Polisi liliwakamata wafuasi wengine wa CHADEMA 145 kati yao wanaume 112 na wanawake 33 wakiwemo viongozi wakuu wachama hicho, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA), John Pambalu, ambao walikamatwa uwanja wa ndege wa Songwe wakiwa tayari wamekwishafika Mkoani Mbeya kwa ajili ya kushiriki kwenye kongamano ambalo lilipigwamarufuku.

“Hivyo, jumla ya watuhumiwa wote waliokamatwa ni 520 na magari 25. Aidha, jumla ya magari 20 aina ya Toyota Coaster yalikamatwa kutoka maeneo mengine kwenda Mkoa wa Mbeya ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam yalikamatwa magari matatu (3), Pwani magari matatu (3), Morogoro magari matatu (3), Iringa magari matatu (3), Njombe magari matatu (3), Songwe magari matatu (3) na Rukwa magari mawili(2).

“Watuhumiwa waliokamatwa walibainika kutoka Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Simiyu, Dodoma, Singida, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Mara na Zanzibar. Watuhumiwa wote walihojiwa kisha kurejeshwa maeneo walikotoka kwa kusindikizwa na Polisi (Police escort),” amesema.

Amesema kwa mkoa wa Mbeya, jumla ya magari matano (5) ambapo Mitsubishi Canter 2, Toyota Coaster 2 na Mitsubishi Fuso 1 yalikamatwa yakitokea Wilaya ya Mbeya, Chunya na Kyela. Watuhumiwa waliokamatwa Mkoa wa Mbeya, wamehojiwa na kupewa dhamana na wengine ambao ni viongozi wa CHADEMA wamerudishwa walikotoka kwa kusindikizwa na Polisi.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kuimarisha ulinzi katika Jiji la Mbeya na Mikoa yote Tanzania ambako wanategemea kufanya vitendo vya uvunjifu waamani ili visifanyike.

Aidha, pia linaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa mbalimbali zinazopangwa kuhusiana na mipango ya kufanya uvunjifu wa amani na yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria bila kujali cheo, wadhifa au itikadi yake.

“Jeshi la Polisi linawataka viongozi wa vyama vya siasa na wafuasi wake kufuata sheria na taratibu za nchi na kuchukua hatua kali za kisheria kwa mtu au kikundi cha watu watakaojihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani,” amesema.

About The Author

error: Content is protected !!