September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Wakulima waathiriwa mvua ya mawe wapata fidia ya mil. 354 kutoka NBC

 

Rais Samia Suluhu Hassan amekabidhi hundi yenye thamani ya Sh 354 milioni iliyotolewa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikiwa ni fidia kwa wakulima wa zao la tumbaku walioathirika na mvua za mawe katika msimu wa kilimo uliopita katika mikoa tofauti hapa nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Fidia hiyo inatokana na huduma ya bima ya kilimo inayotolewa na benki ya NBC kwa kushirikiana kampuni ya Shirika la Bima la Taifa (NIC)

Zaidi,  Rais Samia amekabidhi pia bima ya afya kwa wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao cha mkoani Lindi kupitia huduma ya Bima ya Afya kwa wakulima inayotolewa na benki hiyo kwa kushirikiana na kampuni ya Bima ya Assemble Insurance.

Rais Samia amefanya makabidhiano hayo jana Alhamisi jijini Dodoma alipotembelea banda la NBC lililopo kwenye Maonesho ya Kilimo Nanenane yanayofanyika jijini Dodoma mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Benki ya NBC, Theobald Sabi kuhusiana na huduma mbalimbali za kibenki zinazotolewa na benki hiyo ikiwemo huduma za bima ya kilimo na bima ya afya mahususi kwa wakulima.

“Bima hii ya kilimo ni moja ya suluhisho muhimu katika kuwahakikishia wakulima kipato cha uhakika bila kuhofia changamoto nyingine zikiwemo zile za asili kama vile mvua za mawe. Nitoe wito kwa wakulima nchini kutumia vema fursa hii muhimu kwa kuhakikisha wanapata huduma hizi za bima ya kilimo na bima ya afya. Zaidi nawapongeza sana NBC na wadau wote wanaoshiriki kwenye mpango huu,’’ alisema.

Akifafanua zaidi kuhusu huduma ya Bima ya Kilimo mbele ya Rais Samia, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema itasaidia kuondoa changamato ya hasara walizokuwa wakizipata wakulima kutokana na majanga mbalimbali yaliyo nje ya uwezo wao ikiwemo mafuriko, moto na mvua za mawe ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiathiri ustawi wa wakulima na kusababisha baadhi yao kuhofia kuwekeza kwenye sekta hiyo muhimu.

“Hata hivyo Mheshimiwa Rais hatua hii ya NBC ni mwazo tu kwa kuwa huu ndio mwaka wa pili tangu waanze kutoa huduma hii na tayari mafanikio yanaonekana. Kama serikali tunaahidi kuendelea kuwaunga mkono katika utekelezaji mkubwa zaidi  wa huduma hii lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba huduma hii ya bima ya kilimo inawafikia wakulima wengi zaidi.’’ alipongeza Bashe

Kwa mujibu wa Sabi wakulima walionufaika na malipo hayo wanatoka kwenye vyama vikuu vya ushirika 23 kutoka mikoa ya Shinyanga, Geita, Tabora, Mbeya, Katavi na Kigoma.

“Mbali na huduma huduma hizi za kibima, kama benki kupitia maonesho haya tumeendelea na utaratibu wetu wa kutoa elimu ya fedha na fursa mbalimbali za kibenki kwa wakulima sambamba na kutoa mikopo mbalimbali kwao ikiwemo mikopo ya zana za kilimo hususani mwa matrekta kwa wakilima mbalimbali waliokidhi vigezo na masharti ya mikopo hiyo,’’ aliongeza Sabi.

Akiwa bandani hapo Rais Samia pia alipata wasaa kufahamu huduma mbalimbali zitolewazo na benki hiyo mahususi kwa wakulima ikiwemo Akaunti ya Mifugo inayolenga kuwahudumia wadau wa sekta ya mifugo nchini huku pia akipata  nafasi ya kuzungumza na wanufaika wa huduma hizo akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Lindi Mwambao Bw Hassan Mnumbe ambae chama chake kimekabidhiwa kadi ya bima ya afya kutoka benki hiyo.

About The Author