November 7, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Yunus arejea Bangladesh kuongoza serikali ya mpito

Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Muhammad Yunus

 

MSHINDI wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Muhammad Yunus amerejea nyumbani Bangladesh leo Alhamisi kuiongoza serikali ya mpito ya taifa hilo la Asia. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endele).

Hatua hiyo imekuja baada ya maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi kuhitimisha utawala wa miaka 15 wa Waziri Mkuu, Sheikh Hasina.

Yunus, mwenye umri wa miaka 84, huenda akaapishwa leo jioni kuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo ili kuanza kile mkuu wa majeshi ameapa utakuwa mchakato mzuri sana wa kidemokrasia.

Yunus alilakiwa na mkuu wa majeshi Jenerali Waker-Uz-Zaman, aliyeongozana na wakuu wawili wa jeshi la wanamaji na la angani.

Akizungumza baada ya kuwasili akitokea Paris, Ufaransa, Yunus aliwaomba Wabangladesh kuwa watulivu na kujiandaa kuijenga nchi yao.

Alitoa heshima kwa waliouawa katika maandamano yaliyoiangusha serikali ya Sheikh Hasina, akisema kujitolea kwao kumeipa nchi hiyo ukombozi wa pili.

Yunus, veterani msomi aliondoka Bangladesh mwaka huu baada ya kuwachiwa kwa dhamana katika kifungo cha miezi sita jela kuhusu mashitaka aliyodai yaliyochochewa kisiasa.

Mahakama ya Dhaka hapo jana iliyafuta mashitaka hayo dhidi yake. Jeshi lilikubali masharti ya wanafunzi walioandamana kwamba Yunus, aliyeshinda tuzo ya Nobel 2006 kwa kukuza sekta ya mikopo kwa wafanyabiashara wadogowadogo – aongoze serikali ya mpito.

Licha ya umri wake mkubwa, viongozi wa wanafunzi na makundi mengine ya wanaharakati wanaamini kuwa ndiye mtu anayefaa kuiongoza Bangladesh kuelekea uchaguzi mkuu, na kuondosha uwezekano wa taifa hilo la kusini mwa Asia kuangukia mikononi mwa jeshi.

About The Author