September 19, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mtoto alijeruhiwa shingo na house girl aruhusiwa

 

MTOTO Maliki Hashimu, mkazi wa Goba Jijini Dar es Salaam, aliyekuwa akitibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutokana na majeraha makubwa aliyopata baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mfanyakazi wa ndani ‘house girl’, ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya madaktari kujiridhisha na hali yake. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kitu hicho chenye ncha kali kilitenganisha njia ya hewa chini ya sanduku la sauti na kusababisha ashindwe kupumua, kuongea, kupata maumivu na kupoteza damu nyingi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jumatano kuhusu maendeleo ya kitabibu ya mtoto huyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dk. Rachel Mhavile amesema watalaam wa hospitali wamejiridhisha kulingana na huduma alizopata mtoto huyo tangu alipopokelewa tarehe 15 Julai mwaka huu kuwa sasa yupo salama na ataenda nyumbani ili kuendelea na shule na maisha yake ya kawaida huku hospitali ikiahidi kufuatilia kwa karibu maendeleo yake.

Kwa upande wa wazazi, Baba wa mtoto huyo, Hashim Kitumbi kipekee amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulipa gharama za matibabu ya mtoto huyo, watoa huduma wote wa Hospitali walioshiriki kumhudumia mpaka hatua aliyofikia leo kuruhusiwa, jamii ya watanzania walioguswa na tukio hilo pamoja na vyombo vya habari vilivyofuatilia kwa karibu jambo hilo.

Naye Daktari Bingwa wa Tiba na Magonjwa ya Dharura, Dk. Juma Mfinanga amesema baada ya mtoto huyo kupokelewa akiwa na hali mbaya kutokana na majeraha aliyopata walihakikisha anapata huduma ya kwanza ya kurejesha hali ya upumuaji, kupata damu na badaye kuita timu husika ya wabobezi wa upasuaji wa shingo, pua, koo na masikio.

Dk. Aslam Nkya – Mbobezi wa Upasuaji wa Shingo amesema kwa kushirikiana na timu ya watalaam walimfanyia upasuaji mkubwa mtoto huyo ambao ulichukua muda wa saa nne ili kurekebisha njia ya hewa, sanduku la sauti, matezi yaliyopata changamoto kwenye shingo na kutibu jeraha la nyuma ya shingo.

About The Author