October 13, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Serikali: Hakuna mgonjwa wa Mpox Tanzania

 

Wizara ya Afya imesema kuwa mpaka sasa Tanzania ni salama na hakuna mgonjwa yoyote aliyepatikana na ugonjwa wa Mpox ambao awali ukijulikana kama homa ya nyani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ugonjwa huo ulioanza Mei 2022 hadi kufikia tarehe 31 Mei 2024, wagonjwa 97,745 na vifo 203 vimetolewa taarifa kutoka nchi 116 duniani.

Kaimu mkuu wa kitengo cha mawasiliano serikalini, Englibert Kayombo amesema kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo taarifa za ongezeko la wagonjwa na vifo katika baadhi ya nchi za jirani kama Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aidha, amesema ugonjwa wa Mpox unaweza kusambaa kutoka kwa mtu mwenye maambukizi kwenda kwa mwingine kwa njia zifuatazo; kupitia maji maji ya mwili ikiwemo mate, matapishi, jasho, mkojo; matone ya mfumo wa njia ya hewa; ngozi kupitia kugusana na kujamiana na mtu mwenye maambukizi; ama kutumia vifaa, matandiko au kugusa sehemu zilizo na vimelea vya ugonjwa huu.

Amesema ugonjwa huo unaweza pia kuenezwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.

Kuhusu dalili kuu ya Mpox amesema ni upele, malengelenge au vidonda kwenye mwili hasa mikononi na miguuni, kifuani, usoni na wakati mwingine sehemu za siri. Dalili nyingine ni homa, maumivu ya kichwa, misuli, mgongo, uchovu na kuvimba mitoki.

“Ugonjwa huu haujaingia nchini, hivyo, ni vyema tukashirikiana kuhakikisha nchi yetu inabaki kuwa salama. Wizara inatoa tahadhari kwa wananchi wote kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa wa huu kwa kutoa taarifa kupitia namba 199 bila malipo endapo utamuona mtu mwenye dalili za Mpox.

“Kuepuka kugusa majimaji ya mwili au ngozi ya mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox. Kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana na kubusiana mtu mwenye dalili za Mpox. Kuepuka kugusana na mtu yeyote mwenye dalili za ugonjwa wa Mpox.

“Kunawa mikono kila mara kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono. Epuka kula au kugusa mizoga au wanyama mfano nyani au swala wa msituni. Safisha na kutakasa vyombo vilivyotumika na mhisiwa au mgonjwa pamoja na maeneo yote yanayoguswa mara kwa mara.

“Kuvaa barakoa iwapo itabidi kukaa na kuongea kwa karibu na mtu mwenye dalili za Mpox. Kuwahi katika vituo vya huduma za afya unapoona dalili za ugonjwa wa Mpox. Watoa huduma za afya kuzingatia miongozo ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi (IPC) wakati wote wanapowahudumia wagonjwa,” amesema.
Aidha, amesema wizara imeimarisha ufuatiliaji wa magonjwa hasa vituo vya kusimamia afya mipakani na kuhakikisha vifaa tiba na kinga vipo maeneo ya kutolea huduma.

Pia wataalamu wa afya kwenye maeneo yenye hatari zaidi wanaendelea kupatiwa mafunzo ya kutambua, kutoa huduma pamoja kujikinga.

Aidha, Wizara inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuchukua hatua na kujikinga dhidi ya ugonjwa huu na kuimarisha udhibiti wa ugonjwa huo katika mipaka yote ili kudhibiti Ugonjwa usiingie nchini sambamba na kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa.

Hata hivyo, amesema wizara imejipanga vyema kuhakikisha itatoa huduma bora za matibabu endapo mgonjwa mwenye Mpox atagundulika kuwepo nchini Tanzania.

About The Author