December 13, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Mchengerwa: Kuaminiana kumepunguza migogoro ya wafanyabiashara

 

WAZIRI wa Nchini Ofisi ya Rais Tawala ya Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa amesema kuimarika kwa ushirikiano na kuaminiana kati ya sekta za umma na binafsi kumeongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kijamii sambamba na kupungua migogoro ya wafanyabiashara. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa 15 wa Baraza la Taifa la Biashara jijini Dar es Salaam jana Jumatatu, Mchengerwa ambaye pia ni Mbunge wa Rufiji amesema sambamba na hilo mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji yameimarika katika mikoa na wilaya zake hapa nchini.

“Mikoa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuainisha fursa, changamoto na maoni kwaajili ya kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji,” alisema na kuongeza kuwa miradi ya uwekezaji na shughuli za biashara pamoja na Moradi ya ubia kati ya sekta za umma na binafsi.

Kwa mujibu wa Mchengerwa amesema kwa kuelewa umuhimu wa Mabaraza ya Biashara ya Mikoa (RBCs) na yale ya Wilaya (DCBs), ofisi yake imewezesha kuanzishwa kwa Idara za Biashara, Uwekezaji na Viwanda katika Halmashauri zote.

Alisema katika juhudi za kuhakikisha utendaji wa mabaraza hayo unaboresha, hatua mbalimbali zimeshukuliwa na kuwaongezea jukumu la kufanya mikutano ya mabaraza ya biashara kama majukumu ya wakuu wa mikoa na wilaya ili kuongeza uwajibikaji katika kusimamia majadiliano na maendeleo ya sekta binafsi.

“TAMISEMI imeongeza bajeti za mikoa na wilaya kwa ajili ya kuwezesha shughuli za mabaraza ya biashara na kufuatilia utekelezaji wa maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji. Kwa sasa TNBC imeendelea kugharimia mabaraza hayo,” alisema.

Waziri Mchengerwa alisema TAMISEMI kwa kushirikiana na TNBC wataendelea kuwajengea uwezo wajumbe na wafanyabiashara katika mikoa na wilaya ili waweze kuyasimamia mabaraza ya biashara kwa kuzingatia miongozo iliyopo.

“Tutaendelea kutambua na kutoa tuzo kwa mikoa na wilaya zinazoratibu vyema mabaraza ya biashara na kuvutia uwekezaji,, kukuza uchumi wa eneo husika na kupanua wigo wa walipa kodi na ongezeko la kodi,” alisisitiza.

Katika mkutano wa 15 wa TNBC, Mkoa wa Dodoma uliibuka kidedea na kutunukiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye pia Mwenyekiti wa TNBC tuzo ya mshindi wa kwanza, ambapo mkoa wa Dar es Salaam ulishinda tuzo ya mshindi wa pili na wa tatu.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kibaha, Silivestry Koka (CCM) ambaye pia ni mfanyabiashara alisema kuzinduliwa kwa mkakati maalum wa kidijiti ambao utaazia utaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini.

“Ni hatua kubwa sana kwenye halmashauri zetu kama alivyosema Rais Samia Suluhu Hasan itakuwa chachu kubwa halmashauri zetu. Napenda kuipongeza serikali ya awamu ya sita kwa mageuzi haya,” alisema Koka.

About The Author

error: Content is protected !!