Vikosi vya usalama nchini Venezuela vimetumia mabomu ya machozi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji walioingia mitaani kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi rais Nicolas Maduro. Inaripoti Mitandao ya Kimataifa … (endelea).
Matokeo hayo ya uchaguzi wa juzi Jumapili yanapingwa na upande wa upinzani pamoja na kutiliwa mashaka na mataifa kadhaa ya kigeni.
Maelfu ya waandamanaji walimiminika kwenye mitaa ya mji mkuu, Caracas, wakipiga mayowe ya kudai haki huku wakiapa serikali ya Maduro ni lazima iangushwe.
Baadhi yao walichana mabango ya kampeni yenye picha za Maduro na kisha kuyachoma moto. Sanamu mbili za Hugo Chavez, kiongozi wa zamani wa kisoshalisti ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya muongo mmoja na kumteua Maduro kuwa mrithi wake, ziliangushwa na waandamanaji.
Shirika la Habari la AFP limeripoti kushuhudia maafisa wa usalama wakifyatua mabomu ya machozi na risasi za mpira dhidi ya waandamanaji. Baadhi ya waandamanaji walijibu kwa kuwashambulia kwa mawe.
Maandamano yameripotiwa pia kwenye vitongoji vya wakaazi masikini ambavyo ndiyo vimekuwa ngome ya Maduro na serikali yake ya kisoshalisti.
“Tunataka uhuru. Tunataka Maduro aondoke. Maduro ondoka! amesema Marina Sugey, mkaazi wa maeneo duni alipozungumza na AFP.
ZINAZOFANANA
Ukraine wakiri kufanya mauaji ya Jenerali wa Urusi na msaidizi wake mjini Moscow
Lungu akwama kuwania urais Zambia
Wananchi Comoro wafurahia huduma madaktari wakitanzania