April 8, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Jaji mstaafu Chade: Hatuna dalali

Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mohamed Othman Chande

Spread the love

 

MWENYEKITI wa Tume ya kuchunguza vurugu za uchaguzi mkuu wa 29 Oktoba 2025, Jaji Othman Chande, amekana madai kuwa tume yake inaingiliwa na mamlaka za serikalini nchini Tanzania. Anaripoti Saed Kubenea, Dar es Salaam …(endelea).

“Tume yetu iko huru na haiikingiliwi na mamlaka yoyote. Tume inajitegemea kwa kila kitu. Tume yenyewe ndiyo mhariri, na mamlaka iliyotupa jukumu tutakutana nayo wakati wa kukabidhi ripoti ya mwisho, hatuna mtu yoyote katikati, hatuna dalali,” alieleza Jaji Chande.

Alikuwa akikanusha madai kuwa muda wa kazi ya tume yake umeongezwa ili kuruhusu kuhaririwa kwa ripoti yake.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo, Jumatano, jijini Dar es Salaam, Jaji Chande alisema, tume hiyo ina mamlaka kamili ya mwisho juu ya ripoti yake na haitoi nafasi kwa mtu yeyote kuingilia kazi yake.

Kauli ya Jaji Chande imekuja kufuatia kuibuka kwa madai kutoka kwa baadhi ya wadau hasa wanaharakati mitandaoni, kwamba tume haiku huru na kuongezewa kwake muda mara mbili, kunalenga kutoa nafasi kwa mamlaka fulani ‘kuchakachua’ yaliyomo kwenye ripoti.

Akizungumzia sababu ya kuongeza muda, Jaji Chande alitaja kupanuka kwa wigo wa kazi pamoja na ongezeko la ushahidi unaokusanywa.

“Tulipanga kutembelea mikoa sita, lakini baadaye tukaongeza na kuifikia mikoa 11 na wilaya 22,” alieleza.

Aliongeza kuwa tume imepokea ushahidi mwingi kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, pamoja na ushauri wa kitaalamu ambao unahitaji kuchambuliwa kwa kina kabla ya kukamilisha ripoti.

“Tunachambua ushahidi kwa kina ili kuhakikisha ripoti yetu inakuwa na ubora unaotakiwa, na pia itatolewa kwa lugha ya Kiswahili na tafsiri ya Kiingereza,” alifafanua.

Jaji Chande aliwahakikishia Watanzania kuwa hawapaswi kuwa na hofu kuhusu uadilifu wa ripoti hiyo, akisisitiza kuwa tume hiyo inafanya kazi kwa uhuru bila shinikizo la nje.

Tume iliundwa na Rais Samia Suluhu Hassan 20 Novemba 2025, kuchunguza matukio yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Tume ilipewa siku 90 kabla ya kuongezea siku 42 na tarehe 4 Aprili ikaongezewa tena siku nyingine 21, ambapo sasa itakamilisha kazi yake 24 Aprili 2026.

Minongoni mwa majukumu ya tume hiyo, ni pamoja na kuchunguza kiini cha vurugu za uchaguzi huo zilizosababisha vifo vya watu kadhaa na uharibu mkubwa wa mali zikiwemo ofisi za umma, vituo vya mafuta na vituo vya polisi.

Mashaka ya wananchi ya kuingiliwa kwa tume yanatokana na matamko ya baadhi ya viongozi wakuu wa serikali na chama tawala, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan, waziri mkuu, Mwigulu Nchemba na makamu mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Steven Wassira.

Akizungumza na Wazee wa Dar es Salaam, tarehe 2 Desemba 2025 – siku 10 tangu kuunda kwa tume – Rais Samia alisema, “Nguvu iliyotumika kukabiliana na waandamaji ilistahili.” kwa kuwa walioandamana walitaka kupindua nchi.

Ni kauli hiyo ya Rais, iliyoanza kuchukuliwa na wakosoaji wake, kwamba inalenga kuisukuma tume kulinda maofisa wa serikali waliohusika wa mauaji hayo.

Alirejea tena kauli hiyo, wakati akizungumza na mabalozi, makamishna wakuu na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, Alhamisi ya tarehe 26 Januari mwaka huu, katika mji mkuu wa Dodoma.

Rais Samia alikiri kuwa vurugu zilitokea siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi, lakini akatetea hatua zilizochukuliwa na serikali, akisema madhumuni ya hatua hizo ilikuwa kulinda utulivu wa kikatiba na raia.

Aidha, Rais Samia amewahi kusema pia kwamba waliofanya vurugu walilipwa na watu kutoka nje, huku Waziri Mkuu Mwigulu akidai mara kadhaa kuwa waliofanya vurugu walilipwa na mashirika ya kigeni.

Alisema, “Kuna kijana Mtanzania amelipwa Sh. 5 bilioni ili kuchochea vurugu nchini.”

Naye Wassira alisema, Tume ya Jaji Chande, haichunguzi serikali bali ni kuchimbua chanzo cha ghasia zilizotokea wakati na baada ya uchaguzi wa Oktoba 2025.

About The Author

error: Content is protected !!