SERIKALI ya Tanzania imetangaza bei mpya ya mafuta itakayoanza kutumika kuanzia leo Jumatano, tarehe 1 Aprili 2026. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imeeleza kuwa ongezeko hilo kubwa la bei, limetokana na athari za mzozo wa kivita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
EWURA imesema, mashambulizi katika visima vya mafuta, maghala na viwanda vya kusafisha mafuta Mashariki ya Kati pamoja na kufungwa kwa Lango la Hormuz, kumeathiri gharama za uagizaji wa mafuta nchini.
Lango la Hormuz linapitisha takribani asilimia 20 ya mafuta duniani, na kwamba kufungwa kwake, kumesababisha kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.
Mzozo katika Mashariki ya Kati uliotokana na vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran, uliibuka 28 Februari 2026.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei mpya ya mafuta sasa ni kama ifuatavyo:
Dar es Salaam: Petroli itauzwa kwa Sh. 3,820, dizeli Sh. 3,806 na mafuta ya taa yatauzwa kwa Sh. 3,684.
Tanga: Petroli itapatikana kwa Sh. 3,881, dizeli Sh. 3,867 na mafuta ya taa Sh. 3,745.
Mtwara: Petroli Sh. 3,912, dizeli itauzwa kwa Sh. 3,898 na mafuta ya taa Sh. 3,777 huku maeneo mengine petroli ikiwa ni zaidi ya Sh. 4000.
Taarifa ya EWURA imeeleza kuwa wafanyabiashara wote wa mafuta nchini wanapaswa kuuza bidhaa hiyo, kwa bei zinazoonyeshwa kwenye mabango ya vituo vya mafuta, na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka.
Aidha, EWURA imewataka wananchi kutumia mafuta kwa uangalifu na ufanisi kutokana na athari za kimataifa zinazoendelea.
Bei zilizotangazwa na EWURA, zimekuwa na tofauti kubwa na bei zilizotangazwa tarehe 4 Machi 2026. Katika wakati huo, maeneo mengi bei ilikuwa ni Sh. 2,864 hadi Sh. 2, 959.
Katika hatua nyingine, serikali kupitia EWURA, imeahidi kuchukua hatua za haraka kuhakikisha upatikanaji wa mafuta nchini hauathiriki.
Kupanda kwa bei hizo za mafuta, kumekuja wakati serikali ikisema, kuna akiba ya mafuta ya miezi mitatu nchini na kujigamba kwamba mzozo katika eneo la Mashariki ya Kati, hautaathiri upatikanaji wa mafuta nchini.
Aidha, haijaweza kufahamika mara moja kwamba mafuta ambayo yalikuwa tayari yameshaangizwa yaliwezaje kusababisha kupanda ghafla kwa bei ya mafuta.

ZINAZOFANANA
Bahati haina siku, Jumatano ndiyo siku yako ya kung’ara na Meridianbet
Mwigulu awahakikishia Wana-Isimani kukamilisha miradi iliyoachwa na Lukuvi
Win&Go sasa kubadili mchezo wako, cheza leo, poteza, lipwa kesho