March 30, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Polisi wakana maafa mgodi wa Msasa, Geita

Spread the love

 

UTATA umeiibuka kufuatia Jeshi la Polisi mkoani Geita, kukana taarifa ya kuwapo vifo na majeruhi, katika mgodi wa dhahabu wa Msasa, uliyopo Runzewe, wilayani Bukombe mkoani Geita. Anaripoti Mwandishi Wetu, Geita … (endelea).

Kwa mujibu wa mashuhuda, maafa makubwa yametokea kwenye mgodi huo jana, tarehe 29 Machi, baada ya watu kadhaa kudaiwa kufunikwa na kifusi.

Kifusi hicho kilipomoroka baada ya kutitia kwa maduara na kwamba wengi walioathirika, ni wanawake wanaosaga mawe kwenye eneo hilo.

Vyanzo vya taarifa vinadai kuwa watu kadhaa wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa, kufuatia kuporomoka kwa kifusi kwenye mgodi huo, madai ambayo yamekanwa na jeshi polisi mkoani humo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limekanusha taarifa hizo na kusisitiza kuwa hakuna vifo wala majeruhi waliotokea katika tukio hilo.

Taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Safia Jongo, pamoja na kukiri kutitia kwa maduara manne ya uchimbaji wa madini, katika mgodi wa dhahabu wa Msasa, uliyopo Kata ya Runzewe Magharibi, wilayani Bukombe, mkoani Geita, wakati wa ukaguzi wa kawaida wa maduara yanayofanyiwa ukarabati, “hakuna vifo wa majeruhi.”

“Katika ukaguzi huo, mmoja wa wakaguzi alibaini kibanda kilichikuwa karibu na maduara hayo kimeanza kutitia. Mara moja alitoa tahadhari kwa wenzake waliokuwa ndani ya eneo hilo na wote walifanikiwa kutoka nje wakiwa salama,” imeeleza taarifa ya polisi.

Imeongeza, “Wakati hilo linatokea, maduara hayo hatakuwa katika shughuli za uzalishaji, kwani tayari yalikuwa yakifanyiwa ukarabati.

“Hatua za haraka za kiusalama zimechukuliwa kwa kushirikiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, pamoja na Idara na mamlaka nyingine za serikali kwa ushirikiano wa wananchi. Tathimini ya awali imeibaini kuwa hakuna mtu aliyekuwa ndani ya maduara hayo wakati wa tukio na hivyo, hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokea.”

Hata hivyo, taarifa zilizowanukuu baadhi ya mashuhuda na ripoti kwenye mitandao ya kijamii, zinaeleza tofauti na kilichosemwa na polisi.

Kwamba, wakati tukio linatokea, kulikuwa na mkusanyiko mkubwa wa watu, huku wengine wakidai kuona magari ya wagonjwa yakizunguka kati ya mgodi na kituo cha afya Uyovu, jambo lililoongeza mashaka ya taarifa hiyo.

Kwa sasa, eneo hilo limewekewa ulinzi mkali huku mamlaka husika zikiendelea kufanya tathmini zaidi, na wananchi wakizuiwa kulisogelea kwa sababu za kiusalama.

Akiandika kupitia akaunti yake ya Facebook, Shija Shimbeshi, amedai kuwa kilichoelezwa na polisi, hakina ukweli wowote na kilichotokea ndani ya mgodi.

Mgodi wa Msasa unadaiwa kumilikiwa na baadhi ya vigogo serikalini; na au familia zao.

MwanaHALISI Online linaendelea kufuatilia hatua kwa hatua – Mhariri.

About The Author

error: Content is protected !!