March 30, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

NBC yaendesha kongamano maalum ‘Kuwanoa’ Wanawake Kiuchumi

Spread the love

 

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) imeandaa kongamano maalum lililowakutanisha wanawake wafanyabiashara na wajasiriamali jijini Dar es Salaam, likilenga kuwaimarisha kiuchumi kupitia ubunifu, usalama na ujumuishaji wa kifedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kongamano hilo, lililofahamika kama ‘NBC Women’s Month’, lilifanyika mwishoni mwa wiki ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, inayoadhimishwa tarehe 8 Machi kila mwaka. Mbali na kuwa jukwaa la mafunzo, kongamano hilo pia lilitoa nafasi kwa washiriki kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto na fursa katika uendeshaji wa biashara.

Mkurugenzi wa Masuala ya Uzingatiaji Sheria na Udhibiti wa NBC, Sarah Laiser-Sumaye, aliongoza kongamano hilo lililojumuisha mijadala na mada mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kiafya zilizowasilishwa na wataalamu wabobezi. Washiriki walipata fursa ya kueleza uzoefu wao, hususan namna walivyoweza kukabiliana na changamoto zilizotishia ustawi wa biashara zao pamoja na mbinu walizotumia kunufaika na fursa za mikopo na masoko.

Akizungumza katika kongamano hilo, Laiser-Sumaye alibainisha kuwa changamoto kubwa kwa wanawake wengi si kuanzisha biashara bali ni kuziendesha kwa ufanisi na kuzikuza.

“Pamoja na mafanikio yaliyopo bado kuna biashara nyingi za wanawake zinazokufa kutokana na uendeshaji duni usiozingatia weledi wa kibiashara. Wanawake wengi wanashindwa kutunza kumbukumbu sahihi za kifedha, hivyo kushindwa kutofautisha matumizi binafsi na yale ya biashara,” alisema.

Aliongeza kuwa kupitia kongamano hilo, NBC ililenga kuwakumbusha wanawake umuhimu wa kuboresha uwezo wao katika usimamizi wa biashara, hasa katika maeneo ya utunzaji kumbukumbu na mikakati ya masoko.

Aidha, alieleza kuwa wanawake wengi bado wana hofu ya kurasimisha biashara zao na kuziendesha kwa kuzingatia sheria (compliance), wakihofia gharama za kodi na tozo kutoka mamlaka mbalimbali. Hata hivyo, alionya kuwa hali hiyo inawanyima fursa za kushiriki zabuni kubwa na kupata mikopo rasmi.

Aliwashauri wanawake kujenga utamaduni wa kushirikiana na wataalamu wa biashara ili kuwasaidia katika urasimishaji na uendeshaji wenye tija.

Kwa upande wake, mtaalamu wa elimu ya fedha, Dk. Amina Baamary, akizungumzia mada ya uhuru wa kiuchumi, aliwahimiza wanawake kutumia mikopo kwa uangalifu na kuhakikisha wanazingatia masharti yake.

“Ni muhimu mikopo itumike kwa malengo ya kibiashara ili iweze kuzalisha faida, kukuza mtaji na kuwezesha urejeshaji bila kuathiri biashara,” alisisitiza.

Katika kuimarisha ulinzi wa biashara, wataalamu wa bima akiwemo Moureen Majaliwa kutoka Partner of Pierson Insurance pamoja na Dkt. Milembe Makoye wa Jubilee Insurance Tanzania, walisisitiza umuhimu wa wanawake kuweka kipaumbele kwenye bima za biashara, afya na mali ili kujikinga dhidi ya majanga na changamoto za kiafya.

Naye Meneja wa Bidhaa na Mauzo wa NBC, Dorothea Mabonye, alieleza nafasi ya taasisi za fedha katika kuwawezesha wanawake kufikia uhuru wa kifedha. Aliwahamasisha kufungua akaunti za akiba, akitaja akaunti ya Johari kuwa ni mojawapo ya huduma maalum zinazolenga wanawake.

“Tunatoa mikopo inayolenga mahitaji halisi ya wanawake. Kutokana na changamoto ya dhamana, tumeanzisha utaratibu wa kutumia dhamana zinazohamishika kama magari ili kuwafikia wanawake wengi zaidi,” alisema huku akitaja uwekezaji mkubwa wa huduma za kidigitali katika utoaji wa huduma za benki hiyo kama namna bora zaidi ya kuwafikia wanawake.

Mbali na masuala ya kifedha, kongamano hilo pia liligusa umuhimu wa afya ya akili, ambapo Dk. Roselight Ringo, Mtaalam wa Afya ya akili, aliwasisitiza wanawake kutunza ustawi wao wa kisaikolojia kama sehemu ya mafanikio ya biashara. Aidha, mtaalamu wa mawasiliano ya kimkakati, Carol Ndosi, alitoa mafunzo kuhusu namna ya kujenga utambulisho binafsi na wa biashara (personal branding).

Akishiriki uzoefu wake, mfanyabiashara na mwekezaji katika sekta ya hoteli na kumbi za warsha, Haika Lawere, aliwahimiza wanawake kurasimisha biashara zao ili kunufaika na fursa kubwa za kiuchumi.

“Licha ya umuhimu wa kujiwekea akiba, bado nashauri sana kuhusu umuhimu wa mikopo sahihi kwa kuwa inaweza kuharakisha kasi ya ukuaji wa biashara. Muhimu ni kuwa na nidhamu ya kifedha ili kufikia malengo na kurejesha mikopo kwa wakati,” alisisitiza.

Kwa mujibu wa Meneja Masoko na Mratibu wa Kongamano hilo kutoka NBC, Janeth Mbelwa, alisema tukio ni sehemu ya mkakati mpana wa NBC wa kuwawezesha wanawake kiuchumi, likiwaacha washiriki na maarifa, motisha na mbinu mpya za kukuza biashara zao katika mazingira ya ushindani.

About The Author

error: Content is protected !!