Kabidhi Wasihi Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi
WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imepokea madai 248 kutoka kwa wadau na taasisi mbalimbali kwa iliyokuwa kampuni ya kukopesha fedha ya Pride Tanzania ili waweze kuchakata na kubaini uhalisia wa madai hayo na kuyatolea ufafanuzi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).
Akiongea na waandishi wa habari juma hili jijini Dar es Salaam Kabidhi Wasihi Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi amesema kuwa waliteuliwa na Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Arusha kuweza kusimamia mchakato wa Ufilisi wa taasisi hiyo ya kifedha nchini, na miongoni mwa majukumu yao ni kupata taarifa sahihi za kampuni hiyo kwa kukusanya taarifa za watu wanaodaiwa na wanaoidai kampuni hiyo.
“Mnamo Novemba 7,2025 tulipokea uteuli kutoka mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha kupitia maombi namba 2272 ya mwaka 2025 kuwa mfilisi wa Pride” alisema Kanyusi.
Mara baada ya uteuzi huo wa Mahakama kuu, Januari 26, 2026 Wakala ulitoa notisi kwa umma ya kuwataka wadai wote kuwasilisha taarifa na uthibitisho wa madai yao kwa Wakala ndani ya siku 14 tangu tarehe ya kutolewa kwa notisi hiyo hadi tarehe 8 Februari 2026.
“Kwa majuma hayo mawili tumepokea malalamiko 248 wa madai kwa kampuni hii ya Pride kutoka kwenye makundi mbalimbali ya watu na taasisi nyingine za kifedha kama vile wafanyakazi, mabenki na vikundi vinginevyo vya fedha” alibaninisha Kanyusi.
Pamoja na hayo alibainisha kuwa madai ya wafanyakazi yalikuwa 111 ambayo ni pamoja na malimbikizo ya mishahara, madai ya fedha za usafiri na mengine, lakini pia taasisi nyingine 9 za zabuni zilikuwa zinadai fedha za kusambaza vifaa mbalimbali kwenye taasisi hiyo kwa ajili ya shughuli zao za kila siku.
“Pamoja na hayo tumepokea madai 70, ambayo hayawekwa wazi kuwa wanadai nini katika kampuni hiyo, kwani utaratibu wetu uliwataka wanaodai wote wasema madai yao ni nini na waambatanishe na ushahidi wa madai hayo” alieleza Kanyusi.
Kanyusi alisema kuwa japokuwa kuna wengine hawajawasilisha taarifa za kudaiwa na kampuni hiyo, wao wataendelea na utafiti wao ili waweze kubaini wadaiwa wote wa kampuni hiyo.
Kampuni ya mikopo ya Pride ilisajiliwa rasmi tarehe 5 Mei 1993 kwa lengo la kutoa mikopo isiyo na dhamana kwa vikundi vya wajasiriamali wadogo wadogo wa vijijini ili kuwakwamua kiuchumi.
ZINAZOFANANA
NBC yahitimisha Kampeni Kuhamasisha Kilimo cha Korosho Tandahimba, yakabidhi trekta kwa TANECU
Airtel Africa plc yafanikiwa majaribio yake ya huduma data, ujumbe (SMS) kupitia Starlink
Shinda Samsung A26 leo Jumatano kwa kubashiri rahisi kupitia *149*10#