March 19, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Naibu Waziri Kisuo ahitimisha mashindano ya NBC ya Uandishi wa Insha,  wazo Bora la Biashara kwa wanafunzi

 

NAIBU Waziri wa Kazi, Ajira na Mahusiano Kazini, Rahma Kisuo, amehitimisha rasmi mashindano ya kitaifa ya uandishi wa insha na ubunifu wa mawazo ya biashara kwa wanafunzi wa shule za sekondari, yanayojulikana kama “NBC Essay Challenge” na “NBC Business Idea Competition”, yaliyoandaliwa na Benki ya NBC kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hafla hiyo ilifanyika jana katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wadau wa sekta ya elimu, wakiwemo viongozi waandamizi akiwemo Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Gift Kyando, walimu, wazazi pamoja na maofisa wa Benki ya NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Uendeshaji (COO), Alelio Lowassa.

Katika kipengele cha Wazo Bora la Biashara la NBC, mwanafunzi wa kidato cha tano, Alyah Abdulmajid Ali kutoka Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert, aliibuka mshindi wa jumla na kujinyakulia zawadi ya fedha taslimu Sh. 10 milioni na vitabu vya masomo.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Moses William Tieng’o, mwanafunzi wa kidato cha sita kutoka Sekondari ya Ilboru, aliyepata Sh. 3 milioni, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Wilfred Charles Sengata, mwanafunzi wa kidato cha tano kutoka Sekondari ya Kibaha, aliyepata Sh. 2 milioni.

Nafasi ya nne ilishikwa na Maryam Khatibu Tahiru, mwanafunzi wa kidato cha tano kutoka Shule ya Sekondari ya JKU (Zanzibar), aliyepata Sh milioni 1, wakati nafasi ya tano ilichukuliwa na Mariam Jackson Athumani wa kidato cha sita kutoka Sekondari ya Tambaza.

Kwa upande wa mashindano ya uandishi wa insha, mwanafunzi wa kidato cha tatu, Medard Mussa Elikana kutoka Shule ya Sekondari ya Tabora, alitangazwa mshindi wa jumla na kujipatia zawadi ya fedha taslimu kutoka benki hiyo. Naye mwanfunzi Yasmin Omar Hussein wa Zanzibar commercial alishinda upande wa Zanzibar.

Washindi wengine waliozawadiwa pesa na vitabu ni Shrifra Elisha Mwinuka kutoka Busekelo sekondari, Anne Samwel Jacob kutoka St Ann’s Seminary, Herman Sadiki Asumwisye kutoka Azania Secondari, Gloroa James Mallya kutoka St Ann’s Seminary, Alice Kheri Mwaluko kutoka St Ann’s Seminary na Jonathael John Sarwat kutoka Mzumbe sekondari.

Mashindano hayo yalizinduliwa mwezi Mei mwaka jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda (Mb), yakilenga kuwahusisha zaidi ya wanafunzi milioni moja kutoka shule za sekondari za umma na binafsi nchini. Lengo kuu lilikuwa kuchochea ubunifu, utafiti na uthubutu miongoni mwa vijana, sambamba na kuimarisha elimu ya fedha na ujasiriamali wa vitendo.

Mpango huo ulitekelezwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA) na kampuni ya uchapishaji na usambazaji vitabu ya APE Network.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kisuo aliwapongeza washindi na washiriki wote, hususan waliofanikiwa kuingia hatua ya 15 bora, na kuipongeza Benki ya NBC kwa kuanzisha jukwaa hilo linalowapa wanafunzi nafasi ya kuonesha uwezo wao wa ubunifu na fikra za kiuchumi.

“Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada hizi kwa kuwa zinachangia kwa kiasi kikubwa kuandaa kizazi chenye uelewa mpana wa masuala ya uchumi—kuanzia ubunifu wa mawazo ya biashara, nidhamu ya fedha hadi matumizi sahihi ya taasisi za kifedha kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla,” alisema Kisuo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi, Bi. Lowassa alisema mashindano hayo yamebuniwa kwa lengo la kuwajengea wanafunzi misingi imara ya ujasiriamali, ikiwemo uwezo wa kubuni mawazo bunifu yanayoweza kushindana katika soko la kisasa, kupanga mikakati madhubuti ya biashara na kuzingatia nidhamu ya kifedha.

Aliongeza kuwa mafanikio na muitikio mkubwa uliopatikana katika awamu ya kwanza ya mashindano hayo umeipa benki hiyo hamasa ya kuandaa msimu ujao wenye ubora zaidi na ushiriki mpana zaidi.

“Tunaahidi kuendelea kuboresha mashindano haya ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kuwajengea uwezo utakaowawezesha kushindana katika soko la ajira na biashara,” alisisitiza Lowassa.

Aidha, aliwashukuru washirika wa mpango huo, JICA na APE Network, kwa mchango wao uliowezesha utoaji wa zaidi ya vitabu 2,000 pamoja na zawadi za fedha taslimu kwa washindi.

Baadhi ya walimu na wanafunzi walioshiriki mashindano hayo walieleza kuwa mpango huo umekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea uwezo wa kufikiri kwa ubunifu, kuelewa misingi ya biashara, kuzingatia nidhamu ya fedha na kuthamini utamaduni wa kuweka akiba—stadi muhimu katika kuwaandaa vijana kwa soko la ajira na kujiajiri.

Mbali na Shule ya Sekondari ya Shaaban Robert, shule nyingine zilizofanikiwa kuingiza wanafunzi katika orodha ya 15 bora ya kipengele cha Wazo Bora la Biashara ni pamoja na Tambaza, Ilboru, Minaki, Arusha, Umbwe, Benjamini Mkapa, Jangwani, Azania, JKU (Zanzibar) na Kibaha Sekondari.

About The Author

error: Content is protected !!