MAKAMU wa Rais wa Tanzania,Balozi Emmanuel Nchimbi, ametoa wito kwa wizara zinazohusika na sekta ya mazingira kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwa na mpango wa pamoja utakaowezesha uhifadhi endelevu wa mazingira nchini. Anaripoti Zakia Nanga, Dodom … (endelea).
Nchimbi ametoa wito huo wakati akifanya mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Ashatu Kijaji; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni; Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew; Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Festo Dugange; pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk. Richard Muyungi na wataalamu kutoka wizara hizo katika kikao kilichofanyika mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema wizara hizo zinategemea kwa kiasi kikubwa uhifadhi wa mazingira katika utekelezaji wa majukumu yao. Alifafanua kuwa, kwa mfano, Wizara ya Maji itaweza kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa vyanzo vya maji vitalindwa dhidi ya uharibifu.
Aidha, alibainisha kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yatasaidia kupunguza ukataji miti ovyo na hivyo kulinda misitu iliyopo.
Nchimbi amewasihi viongozi wa wizara hizo kuongeza jitihada ili kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda na kuhifadhi mazingira, akieleza kuwa nchi ina rasilimali nyingi za misitu pamoja na wataalamu wenye uwezo wa kufanikisha malengo hayo.
Ameongeza kuwa tayari Rais Samia amezindua mpango wa kukijanisha nchi na amekuwa akihamasisha upandaji miti mara kwa mara, ikiwemo kutumia siku yake ya kuzaliwa kuhamasisha zoezi la upandaji miti kitaifa.
Kutokana na hilo,Nchimbi amesisitiza kuwa ni muhimu kwa watendaji wote kuongeza bidii katika kuhakikisha Tanzania inakuwa kinara wa uhifadhi wa mazingira.
Nchimbi amewahimiza viongozi hao kuandaa mpango mahsusi wa kukabiliana na changamoto za kuhifadhi miti baada ya kupandwa ili kuhakikisha miti hiyo inakua na kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa na mpango wa kitaifa wa upandaji miti unaokwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani.
ZINAZOFANANA
Jaji Mutungi akutana na Mwakilishi wa UN
ACT Wazalendo yawasilisha wasiwasi wa hali ya kisiasa UN
MO Dewji aendelea kung’ara orodha ya Mabilionea Afrika