March 10, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

MO Dewji aendelea kung’ara orodha ya Mabilionea Afrika

Mohammed Dewji (MO Dewji)

 

RAIS wa Heshima wa Simba na mfanyabiashara, Mohammed Dewji (MO Dewji) ameendelea kung’ang’ana katika orodha wa mabilionea 20 wa Afrika, ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Jarida na mtandao wa Forbes ambayo imetoka tarehe 9 Machi 2026. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Kwa sasa MO Dewji anashika nafasi ya 14 akiwa na utajiri ambao unatajwa kufikia kiasi cha Dola 2.1 bilioni (sawa na Sh 5.4 trilioni) ukichangiwa na uwekezaji katika viwanda vya nguo, unga, mafuta ya kupikia, sabuni, sukari, vinywaji na biashara ya katani.

Mfanyabiashara huyo ni chachu ya kukua kwa MeTL ambapo shughuli zake zimetanuka katika nchi za Afrika zisizopungua 10 zkiwemo Uganda, Ethiopia na Kenya.

Mfanyabiashara huyo mwaka 2016, alitoa ahadi ya kutumia nusu ya utajiri wake katika kutoa uhisani na ufadhili wa kuboresha huduma za kijamii na zinazochochea maendeleo na shughuli za kijamii.

Kabla ya orodha hiyo ya mabilionea ya kwanza kutolewa kwa mwaka 2026, Dewji alikuwa nafasi ya 12 katika orodha ya mwisho kwa mwaka 2025 iliyotoka tarehe 8 Desemba 2025, akiwa na utajiri uliokadiriwa kufikia Dola 2.2 bilioni (sawa na Sh. 5.7 trilioni).

Mo Dewji pamoja na kuwa Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, ndiye mwekezaji wa klabu hiyo ambaye amewekeza Sh. 21 bilioni, huku akisubiri mchakato wa maaadiliko ya klabu hiyo kukamilika.

Mbali na Dewji ambaye ni bilionea namba moja Afrika Mashariki na Kati, mdau mwingine katika mchezo wa mpira wa miguu aliyemo kwenye orodha orodha ya matajiri wa Afrika ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe aliyepanda kwa nafasi moja kutoka ile ya tisa aliyokuwepo Desemba mwaka jana hadi ya nane.

Utajiri wa Motsepe umepanda hadi kufikia kiasi cha Dola 4.3 bilioni (sawa na Sh. 11 trilioni) kutoka ule wa Dola 3.6 bilioni (sawa na Sh. 9 trilioni) aliokuwa nao Desemba, 2025.

Orodha hiyo ya mabilionea Afrika inaendelea kuongozwa na Aliko Dangote wa Nigeria ambaye utajiri wake umepanda hadi kiasi cha Dola 28.5 milioni (sawa na Sh. 74 trilioni).

Itakumbukwa kuwa mwaka 2018, Mo Dewji alitekwa jijini Dar es Salaam katika hoteli moja ya kifahari katika eneo la Oysterbay jijini Dar es Salaam wakati akielekea mazoezini

Hata hivyo mfanyabiashara huyo aliachiwa siku tisa baadae na mpaka ameendelea kuwa miongoni mwa wawekezaji wachache walioajiri zaidi ya Watanzania 25,000 katika kampuni zake.

About The Author

error: Content is protected !!