BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC) ambae ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya NBC jana iliipamba mechi ya Yanga na Simba maarufu kama ‘Kariakoo Derby’ kwa kuandaa matukio kadhaa kwa ajili ya wapenzi wa mchezo huo pamoja na wateja wa benki hiyo. Mechi hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).
Matukio hayo yalilenga kutoa fursa kwa wadau wa mchezo huo wakiwemo wateja wa benki hiyo kukutana pamoja ili kuutazama na kufurahia vizuri zaidi mchezo huo.
Kabla ya kuanza kwa mchezo huo, NBC iliandaa futari maalum kwa wateja wake na wadau wa soka, tukio lililotoa nafasi ya kukutana, kubadilishana mawazo na kuimarisha mahusiano katika mazingira ya kirafiki na kimichezo.
Baadaye, mdhamini huyo aliwawezesha wageni hao kusafiri kwa msafara maalum kuelekea Uwanja wa New Amaan Complex ambako walishuhudia mechi hiyo kutoka jukwaa la VIP kwa hadhi ya kipekee. Pambano hilo lilimalizika kwa sare tasa ya 0-0, lakini burudani na presha ya dabi vilitosha kuwapa mashabiki thamani kamili ya muda wao.

Shughuli hizo ziliongozwa na maofisa waandamizi wa NBC wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Binafsi (wadogo na wakubwa), Elibariki Masuke, ambaye alitumia jukwaa hilo kumkabidhi tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Januari wa Ligi Kuu ya NBC, Pedro Goncalves wa Yanga.
Tukio hilo lilishuhudiwa na maelfu ya mashabiki waliokuwa uwanjani pamoja na mamilioni ya watazamaji waliokuwa wakifuatilia matangazo ya moja kwa moja kupitia televisheni.
Si Zanzibar pekee iliyonufaika na shamrashamra hizo. NBC pia iliweka ‘screen’ kubwa katika maeneo mbalimbali ya mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma, Moshi na Mbeya, kuhakikisha mashabiki wengi zaidi wanapata fursa ya kushuhudia dabi hiyo kubwa zaidi nchini na moja ya mechi zenye mvuto mkubwa Afrika Mashariki.

Nje ya uwanja wa New Amaan Complex, maofisa wa NBC walitoa huduma mbalimbali za kibenki ikiwemo utoaji wa tiketi za kielektroniki, kufungua akaunti na ushauri wa kifedha – wakionyesha kwa vitendo kuwa udhamini wao unaenda sambamba na huduma bora.
Akizungumza wakati wa futari hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano ya Umma wa NBC, Godwin Semunyu, alisema benki hiyo inaendeleza utamaduni wake wa kutumia mechi kubwa kama Kariakoo Derby kujenga na kuimarisha mahusiano na wateja pamoja na wadau wa soka.
“Udhamini wetu hauishii tu kuboresha ligi tunazodhamini, bali pia kuhakikisha wadau wetu – wakiwemo wafanyakazi, uongozi na wateja – wanakuwa sehemu ya moja kwa moja ya mchezo huu. Tunataka soka liwe uzoefu, si tukio la dakika 90 pekee,” alisema.

Aliongeza kuwa NBC inaendelea kubuni mikakati mipya ya kuiboresha Ligi Kuu ya NBC kwa lengo la kukuza vipaji, kuongeza ushindani, kuchochea ajira kupitia michezo na kuimarisha hamasa ya soka nchini.
Katika misimu ya hivi karibuni, imeonekana wazi kuwa udhamini wa NBC umeleta mageuzi makubwa – kuziwezesha klabu kufanya usajili bora, kutoa huduma za kifedha kama bima ya afya na mikopo ya usafiri kwa timu, pamoja na kudhamini hafla za utoaji wa vikombe na tuzo mbalimbali.
ZINAZOFANANA
Sunil Bharti Mittal atunukiwa tuzo ya maisha ya GSMA kwa mageuzi ya sekta ya mawasiliano duniani
Furahia michezo na kasino kwenye Meridianbet Sports Portal leo
Aviator inakupa kubwa kuliko, ushindi wako unakupa Samsung Galaxy A26