February 25, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

RITA yavunja bodi ya wadhamini Kanisa la Waadventista Wasabato

Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Kanyusi

 

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imeivunja rasmi Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista Wasabato Tanzania kufuatia kubainika kwa mapungufu makubwa katika usimamizi wa mali na utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya ripoti ya ukaguzi maalum ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kubaini kuwa bodi hiyo ilishindwa kusimamia ipasavyo mali na rasilimali za kanisa, pamoja na kutotekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Akizungumza Februari 24, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea ripoti ya ukaguzi huo wa kiuchunguzi, Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi amesema kuwa kuvunjwa kwa bodi hiyo ni hatua ya kisheria inayolenga kulinda mali za taasisi na kurejesha nidhamu ya uongozi ndani ya kanisa hilo.

Amesema, pamoja na kuvunjwa kwa bodi, uongozi wa kanisa umepewa siku saba kuwasilisha majina kumi (10) ya waumini watakaopendekezwa kuwa wajumbe wa kamati ya mpito.

Amesema kuwa Kamati hiyo itasimamia mali na shughuli za kanisa hadi pale Bodi mpya ya Wadhamini itakapoundwa kwa mujibu wa sheria.

Kanyusi alieleza kuwa ukaguzi huo maalum ulifanyika kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na baadhi ya waumini wa kanisa hilo katika Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu na kwa Msajili wa Jumuiya za Kiraia chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, wakilalamikia tuhuma za ubadhirifu wa mali za kanisa na matumizi mabaya ya madaraka.

Alibainisha kuwa hatua ya kufanya ukaguzi maalum ilitokana na mashauriano kati ya ofisi yake na Msajili wa Jumuiya za Kiraia katika Wizara ya Mambo ya Ndani, Emmanuel Kihampa, ili kujiridhisha na ukweli wa malalamiko hayo.

“Taarifa hii ya CAG ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha ukweli unajulikana na hatua stahiki zinachukuliwa. Tutaiwasilisha kwa vyombo vingine vya uchunguzi ili wote watakaobainika kuhusika na ubadhirifu au matumizi mabaya ya madaraka wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema Kanyusi.

Kwa upande wake, Kihampa amesema ofisi yake ilipokea malalamiko kuhusu baadhi ya viongozi wa kanisa hilo kushindwa kuwajibika ipasavyo katika usimamizi wa taasisi, hali iliyosababisha sintofahamu na malalamiko kutoka kwa waumini.

Alisema baada ya kupokea malalamiko hayo, ofisi yake ilishirikiana na Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu kuchukua hatua za haraka, hususan kwa upande wa wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na viongozi watendaji wa kanisa hilo.

Hatua ya kuvunjwa kwa bodi hiyo inatarajiwa kuleta uwazi, uwajibikaji na kurejesha imani ya waumini katika uongozi wa taasisi hiyo, huku mchakato wa kuunda bodi mpya ukiendelea kwa kuzingatia matakwa ya kisheria.

Kwa upande wake, Kihamba alisema kuwa ofisi yake tayari imekwisha pokea malalamiko mara kadhaa kutoka kwenye kanisa hilo kutokana na tuhumba mbalimbali za ubadhirifu wa mali za kanisa na kutowasilisha taarifa za kila mwaka.

“Migogoro tunayoiona kwenye taasisi za dini huwa inaanza kama manung’uniko, ambayo yasipofanyiwa kazi kwa wakati hupelekea malalamiko na kuzua migogoro,” alisisitiza Kihamba.

About The Author

error: Content is protected !!