November 23, 2024

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Dk. Biteko: Ubelgiji yaunga mkono ajenda ya nishati safi

 

UBELGIJI imeunga mkono kampeni ya Nishati Safi ya kupikia na hivyo imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika matumizi ya nishati hiyo kwa maendeleo ya Bara zima la Afrika iliyoasisiwa na kinara wa kampeni hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamebainishwa katika kikao cha Naibu Waziri wa Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko na Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Tinne Van Der Straeten kilichofanyika mjini Windhoek, Namibia ikiwa ni sehemu mkutano wa Nchi za Afika kujadili matumizi Hydrojen kutumika katika kuzalisha umeme.

Dk. Biteko amesema ili kupata maendeleo ya kweli, Tanzania inatoa kipaumbele katika matumizi ya nishati ambayo itawawezesha kupata maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja kuondokana na magojwa na vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi.

Amesema ushirikiano wa miaka mingi kati ya Tanzania na Ubelgiji utawezesha upatikanaji wa maendeleo yanayoweza kutokana na uwekezaji wa kimkakati kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji.

“Kama mnavyofahamu, Tanzania kupitia Rais Samia imeasisi na inaendeleza kampeni kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia katika kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia mwaka huu,” amesema Dk. Biteko na kuongeza kuwa:

“Tanzania ingetamani kuungwa mkono na Ubelgiji katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kama ambavyo imekuwa ikifafanya katika sekta nyingine ikiwemo elimu na uwezeshaji katika masuala ya usawa kijinsia.”

Naibu Waziri wa Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko (kulia) akiwa na Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Tinne Van Der Straeten

Kwa upande wake, Waziri Tinne amesema nchi yake iko tayari kuunga mkono jitihada za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni mkakati wa kimataifa wa uhifadhi wa mazingira na kuwawezesha wananchi kukuza pato na maendeleo ya kiuchumi.

Amesema matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati safi ni njia mojawapo ya kuchochea maendeleo ya watu na uchumi wa nchi husika.

Mkutano wa Hydrojen unaoendelea nchini Namibia unalenga kuibua fursa na changamoto zilizopo katika matumizi ya nishati hiyo, ambapo Tanzania itapata fursa ya kujifunza kuhusu matumizi ya Hydrojeni kuzalisha umeme.

Mkutano huo unaohudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi za Afrika unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 5 Septemba, 2024.

About The Author