February 17, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

Airtel yafungua maduka 4 ya kisasa Arusha

KAMPUNI ya Airtel Tanzania imefungua maduka manne mapya ya Smart Shop katika Jiji la Arusha ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kupanua upatikanaji wa mawasiliano ya kidijitali na huduma za kifedha. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Maduka hayo yalizinduliwa rasmi Alhamisi na kaimu mkuu wa wilaya Chausiku Baha ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Jiji la Arusha, Joseph Modest Mkude, alisema Serikali inaendelea kuipa kipaumbele sekta ya mawasiliano kama kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi na mabadiliko ya kidijitali.

Chausiku alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuboresha miundombinu ya mawasiliano na kuharakisha matumizi ya teknolojia za kidijitali ili kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kusaidia ukuaji wa biashara.

Alitaja takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinazoonesha ukuaji endelevu wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya robo ya nne iliyomalizika Desemba 2025, usajili wa laini za simu za mkononi uliongezeka kutoka milioni 99.3 hadi milioni 106.9, huku usajili wa intaneti ukiongezeka kwa asilimia 3.2. Matumizi ya intaneti yaliongezeka kwa asilimia 9.5 katika kipindi hicho.

Ripoti hiyo pia inaonesha kiwango cha matumizi ya simu janja (smartphone penetration) kikiwa asilimia 41.82 na upenyo wa matumizi ya simu kwa ujumla (mobile penetration) ukiwa asilimia 87.11, ukuaji unaochochewa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji unaoendelea katika miundombinu ya mtandao, ikiwemo upanuzi wa huduma za intaneti zenye kasi kubwa kama 5G.

“Ukuaji wa sekta ya mawasiliano umechangia kwa kiasi kikubwa kurahisisha uwekezaji, kusaidia biashara na kuboresha maisha ya wananchi,” alisema Mkude, akiongeza kuwa Arusha inaendelea kuvutia wawekezaji kutokana na soko lake linalokua na umuhimu wake wa kimkakati.

Maduka manne mapya ya Airtel Smart Shop yapo katika maeneo ya Triple A, Morombo, Ngaramotoni na Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA).

Maduka hayo yanatoa huduma mbalimbali ikiwemo mawasiliano ya simu na intaneti, malipo ya kidijitali kupitia Airtel Money, usajili wa laini za simu pamoja na huduma kwa wateja.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Uzoefu wa Wateja wa Airtel Tanzania, Adriana Lyamba, alisema maduka hayo ni sehemu ya mkakati wa kampuni kuwasogezea wateja huduma kupitia vituo vya kisasa vya kidijitali.

Alisema Smart Shop hizo zisizotumia karatasi (paperless) zimeundwa kuongeza ufanisi wa huduma, kupunguza muda wa kusubiri na kuchangia uhifadhi wa mazingira.

“Smart Shop hizi ni za kidijitali kikamilifu, hazitumii karatasi, na zimeundwa kutoa huduma kwa haraka, kwa ufanisi zaidi na kwa kuzingatia mazingira. Hii inaakisi dhamira yetu chini ya kaulimbiu ya ‘Airtel Kila Kona’ kuhakikisha kila Mtanzania anapata mawasiliano ya kuaminika na huduma za kifedha za kidijitali,” alisema.

Lyamba aliongeza kuwa kila duka linatarajiwa kusaidia zaidi ya wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo 400 katika maeneo yanayolizunguka kwa kuwawezesha kupata mawasiliano na huduma za malipo ya kidijitali kwa urahisi, pamoja na kuchangia ajira hususan kwa vijana.

Airtel Tanzania imeendelea pia kuwekeza katika miundombinu ya mtandao mkoani Arusha, ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa minara ya mawasiliano ili kuongeza wigo wa huduma na kuboresha ubora wa mtandao.

About The Author

error: Content is protected !!