February 3, 2026

Mwanahalisi Online

Habari za Uhakika

KESI ZA UCHAGUZI: Wako wapi Wanasheria wa SMZ?

 

KESI tisa za kupinga matokeo ya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi ziliitishwa kwa kutajwa leo kwenye Mahkama Kuu Zanzibar huku upande wa walalamikiwa ukikosa kuwakilishwa. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).

Walalamikiwa kwenye kesi hizo zilizofunguliwa na waliokuwa wagombea uwakilishi kupitia Chama cha ACT Wazalendo, ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar [ZEC] na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambao hawakuwakilishwa kutokana na kutokuwepo hata mwanasheria mmoja wa serikali.

Mbele ya Jaji Salma Ali Hassan, kesi zilitajwa kwa kusomwa shauri Namba 2/2025 linalohusu jimbo la Mwera, Wilaya ya Magharibi A, ambako mgombea wa ACT alikuwa Nassor Ahmed Mazrui, Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa chama hicho.

Jaji Salma aliendesha kesi kwa mazingira hayo huku upande wa walalamikaji ukiwakilishwa na mawakili Omar Said Shaaban na Suleiman Said Abdalla.

Katika hali ambayo upande wa walalamikiwa hawakuwa na wakili wa kuwasimamia mahkamani, Wakili Omar ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa ACT Wazalendo, aliieleza mahkama iangalie namna ya kusikiliza mapingamizi huku wakihitaji nao mahakama kuelekeza upatikanaji wa nyaraka kutoka upande wa walalamikiwa.

Ndipo Jaji Salma alipoitanabahisha mahkama kuwa kwenye jalada la kesi husika hakuna maelezo ya mapingamizi yanayotajwa. Baada ya hapo aliamua kuahirisha kesi na kupanga tarehe 31 Machi kuita kwa kusikiliza mapingamizi hayo.

Kesi za uchaguzi zilipoanza kuitishwa mbele ya Mahkama Kuu mwezi Disemba, upande wa walalamikiwa ukiwakilishwa na jopo la wanasheria serikalini watokao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar. Kiongozi wa jopo alikuwa Mwanasheria Mwandamizi serikalini Said Salim Said, wenzake wakiwa Mbarouk Suleiman Othman, Ali Issa Abdalla na Maulid Makame Ame anayewakilisha Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar [ZEC]. Haikufahamika sababu za kutofika kwao leo wala kutojitokeza mwanasheria yeyote wa serikali.

Kesi tisa zilizotajwa leo mbele ya Jaji Salma, ni za majimbo ya Mwera, Welezo, Amani, Mpendae, Mtoni, Bumbwini, Kijini, Nungwi na Tumbatu.

Majimbo mengine manane kwa Unguja ambayo matokeo yale yanabishaniwa ni Pangawe, Mwanakwerekwe, Malindi, Kiembesamaki, Chumbuni, Chaani, Mkwajuni na Makunduchi.

Tayari kesi zake zimetajwa mbele ya Jaji Mohamed Ali Mohamed Shein, na kuakhirishwa hadi tarehe 24 Februari 2026 zitakapoanza usikilizaji wa mapingamizi yaliyowekwa na walalamikiwa.

Maeneo ambayo yamewekewa vizingiti ni kasoro za viapo, kutofuatwa miundo na taratibu, kutomaliza taratibu nyengine za kisheria.

About The Author

error: Content is protected !!